Serikali: Chanjo 2 corona zipo nchini

22Jul 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali: Chanjo 2 corona zipo nchini

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema chanjo zimefika nchini na anayehitaji kuchanjwa yupo huru kuchanjwa wakati wowote katika hospitali maalumu kwa huduma hiyo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza katika Baraza la Eid El Adha, lililofanyika kitaifa kwenye Msikiti wa Mtoro, Kariakoo jijini Dar es Salaam, jana. PICHA: OWM

Amesema serikali ilichukua uamuzi wa busara wa kuagiza na kuziletea chanjo nchini baada ya kugundua kuna Watanzania ambao ni wafanyabiashara na wasafiri wa shughuli tofauti nje ya nchi, ambazo sharti upatiwe au kuwa na cheti cha chanjo kuingia nchini mwao.

Waziri Mkuu pia amesema jamii izingatie lishe na mfumo uliotumika mwaka jana katika kuimarisha kinga kwa kula malimao pamoja na matunda uendelee kupambana na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Majaliwa ametoa wito huo jana katika Baraza la Eid El Hajj, lililofanyika katika Msikiti wa Mtoro, Ilala jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kila Mtanzania kuliombea taifa ili kujinusuru na ugonjwa huo ulioathiri zaidi mataifa mengine.

“Chanjo ipo, anayetaka akachanje, hospitali zimeelezwa mahali zilipo, nenda, ni kinga pia. Juzi nikiwa Morocco, hii ni nchi rafiki na Tanzania, lazima uwe umepima mara kadhaa, vipimo vikionyesha upo vizuri, sawa.

“Katika salamu za Eid nilisema hili, muhimu kwa Watanzania. Kuna Watanzania ambao wanataka kwenda huko wakatimize haja zao, tukaona utafiti ufanyike ili kuona wenzetu wamechanja ipi, ambayo haina madhara kwa kiasi kikubwa… tukabaini ipi nzuri tumepata mbili kati ya zote.

“Kuna Watanzania walikwenda hata Afrika Kusini kuchanja. Tumezileta nchini kila anayehitaji apate fursa ya kuchanjwa, badala ya kufanya mtu aende nje ya nchi," alisema.

Majaliwa alisema pamoja na kuimarishwa mahitaji kwa mahitaji muhimu ya kupambana ugonjwa huo katika maeneo tofauti ikiwamo mipakani, alisisitiza kila mmoja kuchukua tahadhari ili kukabiliana na corona.

“Nchi zetu za jirani zinakabiliwa na ugonjwa huu sana kuliko sisi, hatujazuia mipaka ili kuruhusu kila mmoja na Watanzania kujitafutia riziki, wapo tunaowatambua baada ya kuchunguzwa maeneo fulani, lakini wapo walioambukizwa na corona na hatujawatambua.

“Tufuate kanuni kwa kuendelea kunawa mikono, hapa msikitini nimeona kabla ya kuingia tunanawa mikono, ila tuongeze sabuni miminika kabla ya kuingia msikitini tuchukue tahadhari.

“Waislamu hatujamudu kwenda Makka, kwa ajili ya hija, wenyeji wetu wamesema hapana, nchi chache ambao wao wanaamini walijizatiti kwa chanjo walikwenda, bado kuna maambukizi, watu wake ambao wana chanjo.

“Ukijua upo chini ya mita moja kutoka kwa mwenzako, ukiingia msikitini, vaa barakoa. Ugonjwa huu huwapata zaidi walio na miaka 45 na kuendelea.

"Tuzingatie yanayopunguza maambukizi, kufanya mazoezi ili utoke jasho, kwa kutembea umbali mrefu afya inapokuruhusu, mazoezi hata kuzunguka nyumba yako yanatosha," alisema.

Majaliwa pia alitoa rai kwa viongozi wa dini na waumini waendelee kuvumiliana, kustahimiliana na kushikamana na kufanya ibada, kuienzi tunu ya amani bila kujali itikadi za dini na kwamba Tanzania imekuwa nchi kimbilio la waliokosa amani kwa kuwa ina amani.

“Tuendelee kufanya ibada, kuwaombea wenzetu waliotangulia mbele za haki, tuonyeshane upendo na mshikamano hata baada ya kumalizika kwa siku 10 bora ya Dhul Hijja.

“Kila Mtanzania anao mchango mkubwa katika kutunza na kuimarisha amani ya nchi, hivyo wananchi wote tuendelee kuitunza tunu hiyo," alihimiza.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir Bin Ally, aliwataka Watanzania kuendelea kuimarisha maadili mema.

“Tumwombe Mwenyezi Mungu ili tuondokane na majanga yanayoikabili nchi yetu na dunia nzima," alisema na kuwataka waumini wa Kiislamu na watu wote kwa ujumla kufuata mafunzo ya dini yanayotilia mkazo maadili mema na mshikamano.

“Taifa lolote likiwa halina maadili lazima litaporomoka, taifa lolote ni tabia tu, tabia nzuri litaendelea, Watanzania tukiendeleza kudumisha maadili mazuri, tutastawi na kuendeleza nchi yetu," alisema.