Serikali kuagiza mitambo 25 ya kuchimba visima

19Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali kuagiza mitambo 25 ya kuchimba visima

SERIKALI inatarajia kuagiza mitambo mikubwa ya kisasa 25 ya uchimbaji visima na seti tatu ya mitambo ya kujenga mabwawa lengo likiwa ni kutoa huduma kwa wananchi mjini na vijijini na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji nchini.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa, Simon Ngonyani katikati akizungumza na wafayankazi wa kitengo hicho leo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es salaam, katika Ofisi za Kitengo cha Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa zamani ikijulikana kama Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA), Mkurugenzi mpya wa kitengo hicho kilichopo chini ya RUWASA, Simon Ngonyani, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wengi mjini na vijijini.

"Hivi sasa uchimbaji visima umeingiliwa na watu ambao ni vishoka, lazima tuwaambie wananchi pamoja na taasisi ambazo zinahitaji huduma ya kuchimbiwa visima,hawana sababu ya kutangatanga mitaani waje DDCA ya zamani ambayo sasa imebadilishwa jina kwa na kuitwa Kitengo cha Uchimbaji Visima na Mabwawa tuwapatie huduma kwani kitengo chetu kina wataalam wa kutosha wenye uwezo wa kazi hiyo," amesema Ngonyani 

Amesema mwaka jana walipewa kazi na Wizara ya Maji ya kuchimba visima 500, lakini walishindwa kukamilisha kazi hiyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mitambo ila kwa mwaka huu wanaimani watafanikiwa kuchimba visima zaidi baada ya serikali kuagiza mitambo hiyo.

Ngonyani, ametahadhrisha wananchi,taasisi za umma na serikali kuacha kutumia vishoka kwani hawana utaalam. "Kwa mfano ukiangalia kwa hapa Dar es salaam, utakuta visima vingi vimechimbwa karibu na miundombinu ya majitaka na kusababisha magonjwa ya milipuko. Kumbe watu wanatumia maji yanayoingiliana na mfumo wa maji machafu," amesema.

Habari Kubwa