Serikali kuajiri walimu 12,000

05Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Serikali kuajiri walimu 12,000

SERIKALI imesema iko katika mchakato wa kukamilisha taratibu za kuajiri walimu wapya 12,000 kwa ajili ya shule za msingi na sekondari nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo, alitangaza taarifa hiyo njema kwa kada hiyo alipohutubia kwenye Siku ya TAMISEMI jijini hapa na kubainisha mafanikio kwa kipindi cha miaka mitano katika sekta ya elimu.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano, walimu zaidi ya 18,000 wameajiriwa na kupelekwa shule za msingi na sekondari na kwamba wanaendelea na mchakato wa kutoa ajira zingine 12,000 zilizoelekezwa na Rais John Magufuli.

“Ninafahamu bado kuna changamoto ndiyo maana Rais alitoa maelekezo ajira za walimu zingine zitolewe na ametoa maelekezo ya ajira zaidi ya 12,000, taratibu zinaendelea, zitakapokamilika mtasikia tunaongeza ajira zingine kwa shule za msingi na sekondari,” alisema.

Jafo alisema serikali imejipanga kununua magari kwa ajili ya maofisa wa elimu wilaya nchini, ili kurahisisha utendaji kazi wao.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mitano, Jafo alisema kwa kipindi hicho kiasi cha Sh. trilioni 1.09 zimetolewa kwa ajili ya kugharamia mpango wa elimu bila malipo.

Jafo alibainisha kuwa Sh. bilioni 502 zimetolewa kwa ajili ya shule za msingi na Sh. bilioni 593.9 zimeenda sekondari, jambo ambalo limesaidia watoto wa maskini kupata elimu.

“Mwaka 2016 ,watoto wengi walifurika kwenye shule zetu. Wakati zikiwa zimekadiria watoto 200 hadi 400, zingine zilisajili hadi wanafunzi 1,000. Kwa mfano, Shule ya Nyakanazi na Majimatatu zilikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi, watoto wengine walisajiliwa wakiwa na miaka 10 kutokana na miaka mitatu nyuma walikosa fursa hiyo,” alisema.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano, zaidi ya Sh. bilioni 501 zimetolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali.

Alisema hadi kufikia Juni 2020 mwaka huu, ujenzi wa shule mpya za msingi 905 ulikuwa umekamilika, hivyo kuongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020.

Waziri huyo pia alisema vyumba vya madarasa 17,215 vimejengwa na kuongeza idadi kutoka vyumba 108,504 mwaka 2016 hadi 125,719 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 13.7.

Alisema serikali inaendelea na ujenzi wa vyumba 3,049 na ukikamilika, idadi ya vyumba vya madarasa kwa shule za msingi itafikia 128,768.

Jafo alisema serikali pia imepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa madawati kutoka kuwa na madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi kufikia 8,095,207 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200.

Alisema serikali imejenga shule mpya za sekondari 228 na hivyo kuongezeka kutoka shule 4,708 mwaka 2016 hadi 5,330 mwaka 2020.

Alisema vyumba 227 vya maabara za masomo ya sayansi vimekamilishwa kwa gharama ya Sh. bilioni 2.63, ujenzi ambao umeongeza idadi ya vyumba vya maabara kutoka 4,237 mwaka 2015 hadi 4,464 mwaka 2020.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Joseph Nyamhanga, alisema uwekezaji na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari umesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutoka asilimia 67.84 mwaka 2015 hadi asilimia 81.50 mwaka 2019.

Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli, alisema mpango wa elimu bila malipo ulianzishwa mahsusi baada ya utafiti walioufanya mwaka 2014 kuonyesha kuwa watoto milioni 3.5 walikuwa nje ya shule kutokana na kukosa ada.

"Sasa, mafanikio haya tunayoyaona ni matokeo ya uamuzi wa Rais Magufuli alioufanya mwaka 2015 mwishoni hadi Januari 2016 ya kuanzisha mpango wa elimu bila malipo,” alisema Mweli.

Habari Kubwa