Serikali kuanzisha wakala wa kilimo cha ‘Horticulture’

19Nov 2019
Godfrey Mushi
ARUSHA
Nipashe
Serikali kuanzisha wakala wa kilimo cha ‘Horticulture’

MCHAKATO wa Serikali kuanzisha Wakala wa Maendeleo ya Kilimo cha Maua, Mboga, Matunda na Viungo maarufu kama ‘Horticulture’ ili kuchochea mkakati mpya wa kufikia mapinduzi ya kijani, umeiva.

Jana, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema wakala huyo atajulikana kama ‘Horticulture Development Agency’ (HDA).

Kwa mujibu wa Bashe, mchakato huo utakuwa umekamilika rasmi ifikapo Februari mwaka 2020, ukilenga zaidi kuchochea ukuaji wa sekta ndogo ya kilimo hicho. “Wakala wa Maendeleo ya Kilimo cha Maua, Mboga na Matunda atasaidia kuondoa vikwazo vyote vinavyokwaza sekta hii ndogo, lakini yenye manufaa makubwa na kuchochea ukuaji wake kwa kasi,”alisema Bashe.

Naibu Waziri Bashe, alidokeza kuhusu mchakato huo, baada ya kukutana na wadau wa sekta hiyo wakiongozwa na Taasisi Kilele ya Kilimo hicho yaani Tanzania Horticultural Association (TAHA). Chombo hicho kinachotarajiwa kuibeba sekta hiyo, kinatajwa kwamba kinapaswa kuchangia kwenye uchumi wa taifa kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.85 kwa mwaka ifikapo mwaka 2021.

Mchango huo wa sekta ya matunda na mboga utakuwa umepanda kutoka dola milioni 764 za Marekani inayochangia kwa sasa na kuajiri vijana na wanawake kwa wingi. “Serikali imeamua kwa makusudi kabisa kuipa kipaumbele sekta ndogo ya horticulture ambayo inakua zaidi ikilinganishwa na kilimo cha mazao mengine ya biashara kama pamba, kahawa, korosho, tumbaku na mengine,” alisema Bashe  Takwimu za Wizara ya Kilimo zinaonyesha kuwa sekta ndogo ya horticulture inakua kwa asilimia 11, wakati sekta nzima ya kilimo inakua kwa takribani asilimia nne tu. Bashe alisema kuwa Wizara ya Kilimo inabadilisha sheria kwa lengo la kuunganisha mamlaka za udhibiti ili kupunguza urasimu, kurahisisha taratibu za kusafirisha mazao nje ya nchi na kuwapunguzia mzigo wa tozo wakulima wa horticulture. “Tutahakikisha tunarahisisha uingizwaji wa teknolojia za kisasa ili kuinua kilimo cha horticulture, usafirishaji wa mazao, uboreshaji wa miundo mbinu na pia kutenga maabara tatu maalumu kwa ajili ya kupima mazao ya horticulture kwa ajili ya masoko ya nje, ”alisema Naibu Waziri huyo Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dotto James aliitaka TAHA kuandaa orodha ya kodi sumbufu na kuziwasilisha kwenye kikosi kazi cha bajeti cha Wizara ya Fedha kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi ikiwamo kufutwa. Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha, aliitaka TAHA kuangalia uwezekano wa kukodisha ndege kwa ajili ya kusafirisha mazao hayo nje ya nchi na kwamba serikali itasaidia mpango huo wakati inaangalia uwezekano wa kununua ndege maalumu ya mizigo. Naye, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Masoko wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Lydia Mallya alisema wanafikiria kuanzisha kitengo maalumu cha kuhudumia mazao ya horticulture bandarini kwa ufanisi zaidi. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo na Mifugo, Mahmoud Mgimwa, alisema kamati yake itafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kusaidia kukuza kilimo cha horticulture. Awali, akiwasilisha matatizo na fursa za sekta ndogo ya horticulture, Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA, Jacqueline Mkindi alisema mkulima aliyerasimisha shughuli zake za kilimo analipa kodi na tozo mbalimbali zipatazo  47 kwa mwaka, jambo ambalo ni mzigo mzito kwa mkulima. Mkindi alisema: "Ili kukuza horticulture kwa kasi, serikali inapaswa kuboresha mazingira ya kufanya biashara, kubadilisha sheria ya mazao, kurahisisha usajili wa viwatilifu vinavyohitajika kwenye mazao ya mboga, matunda na maua.  “Kama nchi tunahitaji kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kilimo cha horticulture." Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi huyo wa TAHA, alisema kuna uhitaji wa kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa mifumo wa usafirishaji wa mazao ya horticulture katika viwanja vya ndege na bandarini ili mazao hayo yasiharibike kwa ucheleweshwaji. Kuhusu suala la mafunzo, Mkindi aliiomba serikali kusaidia uanzishwaji wa vyuo binafsi vya mafunzo ya kilimo cha horticulture kwa vitendo, kuboresha mitaala ya kufundishia wataalamu wa kilimo hicho katika vyuo vya Horti-Tengeru na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na pia kurahisisha utoaji wa vibali vya kufanya kazi kwa wataalamu kutoka nje.

Habari Kubwa