Serikali kuboresha sheria ya uwekezaji

10Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali kuboresha sheria ya uwekezaji

SERIKALI imeanza kufanya maboresho ya sheria na sera ambazo zitachochea kuwapo kwa mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na
wawekezaji, hivyo kufikiwa kwa wakati azma ya uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, PICHA MTANDAO.

Akizungumza wa mkutano wa majadiliano baina ya serikali na sekta binafsi uliolenga kuangazia changamoto mbalimbali za wafanyabiashra na wawekezaji nchini mwishoni mwa wiki Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, alisema serikali ya Rais John Magufuli imejielekeza kuzifanyia kazi sera na sheria za uwekezaji.

“Azma ya serikali ni kujenga uchumi wa kati na viwanda, hatuwezi kufika huko kama wadau wa maendeleo kutoka sekta binafsi wanakuwa waathirika wa sheria zetu. Serikali imekusudia kuleta mabadiliko hayo ili kupunguza kiwango cha tozo, kodi na kiwango cha usajili katika Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC),’’ alisema na kuongeza:

“Mapendekezo ya maboresho ya sheria ya uwekezaji yanategemewa kuwasilishwa mapema kwenye bunge lijalo.”

Waziri Kairuki alisema amefarijika kwa namna ambavyo wawekezaji na wafanyabiashara walivyoitika wito wa kuja kwa wingi katika majadiliano hayo katika mikoa yote waliyopita mpaka sasa jambo ambalo limewapa mawanda mapana katika kushughulikia changamoto za wawekezaji.

“Mwitikio ni mkubwa jambo ambalo linaonesha ni kwa namna gani Tanzania tumepiga hatua katika kuwavutia wawekezaji, tutazifanyia kazi changamoto zote ambazo zimeibuliwa na wadau wa sekta binafsi hali ambayo itaongeza idadi ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,’’ alieleza.

Katika hatua nyingine Waziri Kairuka aliagiza mabaraza ya biashara ya mikoa na taasisi zote zinazohusika na uwekezaji kutoka
maofisini na kufika kwa wananchi ili kuendelea kutoa elimu juu ya mambo mbalimbali ambayo yamekuwa changamoto kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

“Hatuwezi kufika popote kama wataalamu wetu watabaki maofisini, huku wawekezaji na wafanyabiashara wakihangaika kwa namna wanazojua wao, natoa maagizo kwa idara zote za serikali zinazohusika na uwekezaji kuwafikia walengwa popote walipo ili kuwarahisishia ufanyaji wa shughuli zao hapa nchini,’’ alieleza.

Waziri Kairuki alielezea kulidhishwa na kazi zinazofanywa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) hasa katika kuratibu na
kuyasimamia mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya kwani yana mchango mkubwa kwa maendeleo na ustawi wa uchumi.

Waziri Kairuki aliongeza kuwa changamoto kubwa waliyokutana nayo kwa wafanyabiashara ni kutokuwa na ufahamu juu ya uwasilishaji wa changamoto wanazokumbana nazo kwenye shughuli zao jambo ambalo linaitia doa serikali wakati taasisi zinazosimamia uwekezaji zipo.

“Changamoto zingine sio za kisera wala sheria, ni za watu wachache kutoka kwenye taasisi zilizopewa jukumu la kusimimia uwekezaji, serikali haitakubali kuvumilia watu wa aina hiyo na itawashughulikia kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma,’’ alifafanua.

Habari Kubwa