Serikali kuchukua hatua uvamizi nzige

02Mar 2021
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Serikali kuchukua hatua uvamizi nzige

SERIKALI inafuatilia ‘kusuasua’ kwa Shirika la Nzige wa Jangwani kupambana na kundi jipya la nzige lililoingia nchini wilaya za Longido na Monduli mkoani Arusha, na kuahidi kuchukua hatua kama shirika hilo halitaongeza juhudi.

Jana, Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, alisema amezungumza na Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, kuhusu suala hilo, kutokana na Tanzania kutoridhishwa na utendaji wa shirika hilo.

Mara ya kwanza nzige zaidi ya milioni 50 waliripotiwa kuingia nchini Februari 19, mwaka huu, kupitia Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro na baadaye kuelekea baadhi ya maeneo ya vijiji vya wilaya ya Same na Simanjiro, mkoani Manyara.

“Tumeongea na Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi wetu kule Ethiopia atakuwa amemwita Mkuu wa shirika hili, kumweleza kwamba tungependa tuone kweli wako makini zaidi, na sisi ni wanachama na tumelipia fedha na Tanzania ni kati ya nchi mbili ambazo zimelipa ada yote ya uanachama. Ndege za shirika hili ni ndege zetu sisi wote, lakini hili shirika lina ndege iko Moshi, muda wote imetua wamemchukua rubani wamempeleka Kenya.”

“Nimejaribu sana kumpigia simu, Mkuu wa shirika hili simpati, ameambiwa kwamba namtafuta na amepewa namba yangu hajanipigia simu. Kwa hiyo nampelekea tu salamu kwamba haturidhishwi na utendaji wake, sisi kama wanachama na inawezekana kama uzembe ni wa kiasi hiki ambacho nimeuona, si ajabu kwamba tukaona hii shughuli ya kupambana na nzige wa jangwani, bado inaendelea kuwa changamoto.

“Kwa hiyo tunataka tuone hili shirika likifanya kazi vizuri, tumetoa pesa zetu za Watanzania na tunajua wanapata misaada kutoka mashirika mbalimbali, waongeze juhudi. Haiingii akilini kwa nini kuna ndege iko Moshi imetua muda wote bila kumwaga viuatilifu, lakini hairuki kwa sababu wao wamemchukua rubani aliyekuwa hapa na wamempeleka Kenya.”

Prof. Mkenda alisisitiza: “Kwa hiyo tutaendelea kulifuatilia hili na tutachukua hatua madhubuti kama uongozi wa shirika hili hautaongeza juhudi za kupambana na nzige. Lakini kwa ujumla napenda kuwahakikishia Watanzania kwamba tuko makini sana na tunatumia capability zote (nguvu), kuwamaliza nzige hawa na mpaka sasa hivi hatujapata madhara ya aina yoyote kutokana na nzige walioingia hapa Tanzania.”

Kwa mujibu wa Waziri Mkenda, sasa hivi kuna kundi jipya limeingia kutoka Kenya ambalo lipo Longido.

“Kwa Wilaya ya Siha (Kilimanjaro), tumewateketeza wale ambao walikuwa wameingia, lakini kakundi kadogo kaliescape (kalikimbia) kakarudi Longido, baada ya kukaa na kufuatiliwa, wakaruka wameenda Monduli. Kundi hilo sasa hivi wataalamu wako pale wanalifuatilia kwa ajili ya kuliangamiza.

“Kuna kundi jipya la nzige wachanga sana limeingia kutoka Kenya, limeingia Longido na sasa hivi tunajua mahali lilipo, tunasubiri kwenda kuliteketeza. Tuna helikopta inaweza ikaondoka muda wowote kutokea Uwanja wa Ndege wa Arusha, kwa ajili ya kwenda kumwaga viuatilifu pale na itaenda tena Wilaya ya Monduli.

Prof. Mkenda alisema nzige wengi wamekufa baada ya kunyunyuziwa dawa aina ya Fenitrothion 96% ULV, kwenye maeneo ya mapori na nzige hao walitua makundi kwa makundi.

Vile vile, amesema kuna kundi moja liko Simanjiro ambalo wanaendelea kuliteketeza, lakini kwa sababu ya mazingira ya Simanjiro, wamepata shida kwa sababu limeingia maeneo yenye miiba na vichaka vikubwa, na wataalamu waliopo huko wanashindwa kulielewa sasa hivi liko wapi.

Waziri Mkenda, amedai kuwa kuna dalili kwamba huenda likawa limevuka kwenda Wilaya ya Kiteto au bado liko Wilaya ya Simanjiro.

WAOMBA NDEGE TANAPA

Wakati vita dhidi ya nzige hao wa jangwani ikiwa imeshika kasi, Waziri Mkenda, alisema tayari wizara yake imeomba ndege ndogo ya ufuatiliaji ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kusaidia kwenda kuangalia angani kundi hilo ili baadaye helikopta iende ikawapige sumu nzige hao mahali popote walipo.

“Tumeongea vile vile na Wizara ya Maliasili na Utalii, kuwaomba kwamba zile Hifadhi za Taifa zote pamoja na misitu ya serikali ambayo iko mpakani, wafanyakazi waliopo kule na wenyewe wawe macho, waangalie kama kuna kundi lolote litakuwa linaingia na maeneo ambayo hakuna wananchi ambao wanatupa taarifa, basi watupe taarifa tuende tukapambane nao.

“Ndege ya Survilance ya TANAPA (ndege ya ufuatiliaji), haiwezi kunyunyuzia, lakini itakuwa inaongeza nguvu, kwa ajili ya kuruka kuangalia maendeleo yanavyoenda.”

HELIKOPTA YA NZIGE WEKUNDU

Waziri Mkenda alisema pia serikali imeleta helikopta kutoka Shirika la Kupambana na Ndege Wekundu nchini Zambia.

Alisema kwa kuwa ndege hiyo ni wanachama wote wa shirika hilo na tayari imeshaondoka Zambia na imeshatua nchini.

Jana (juzi) ilikuwa inafanya ufuatiliaji na leo (jana) ilikuwa inanyunyiza sumu katika maeneo ya Longido na Monduli.

“Tunaendelea kufuatilia nini kinaendelea katika mwenendo wa nzige, tunafuatilia sana juhudi za Kenya za kupambana na nzige hawa na tunawasiliana nao. Nafurahi kusema kwamba hata kuna kundi moja lilikuwa linavuka mpaka, lakini lilishambuliwa na Kenya na kuteketezwa. Wenzetu nao kule (Kenya) wamerusha ndege kuhakikisha kwamba wanaua nzige hawa kama ambavyo sisi tunafanya upande huu,” alisema.

UPEPO MBAYA

Alisema wamepata taarifa kwamba kuna kundi jingine linakuja kutokea Machakos, hivyo upepo unaweza ukawa unawaleta kupitia upande wa Kajiado kuja Tanzania.

Prof. Mkenda alisema kuwa tayari wameshawasiliana na Kenya, wakitaka kuliwahi kundi hilo kuliangamiza.

“Tunajua nzige hawa wanasafiri kilomita 80 kwa siku na wakishafika wanatua. Mara nyingi tunawashambulia wakiwa chini, kwa jioni wanatua wanalala, asubuhi kwa ndege unaweza ukawapiga au ukawahi ukawapiga jioni.

Hizi ndege ni ndogo na wakati mwingine hatuzitumii kumwaga sumu jioni, kwa sababu haziruki kwenye giza, ndio maana jioni tunawatumia wanaokuwa na pampu za mkono.

Hizi juhudi tunazofanya sasa hivi mtashangaa kwa nini tumechukua ndege helikopta kutoka Shirika la Kupambana na Nzige Wekundu lenye makao makuu yake Zambia, ambalo sisi ni wanachama na tunalipia, wakati nzige hawa sio nzige wekundu, hawa ni nzige wa jangwani na sisi vile vile ni wanachama wa Shirika la Kupambana na Nzige wa Jangwani, lenye makao makuu Ethiopia.”

Habari Kubwa