Serikali kudhibiti uuzaji holela wa vitunguu saumu

10Sep 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Serikali kudhibiti uuzaji holela wa vitunguu saumu

SERIKALI imesema inaendelea kudhibiti uuzaji holela wa vitunguu saumu kwa kutumia magunia ya lumbesa,mabeseni na ndoo ili mizani itumike katika minada ambayo hufanyika katika ghala la vitunguu saumu bashay wilayani Mbulu.

Aidha, Baadhi ya mataifa ambayo hununua vitunguu saumu vinavyozalishwa nchini ni Shelisheli, Visiwa vya komoro, Msumbiji, Zambia, Mauritania, Kenya, Uganda na Falme za kiarabu.

Hayo yameelezwa leo bungeni na Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini(CCM), Flatei Massay.

Katika swali lake, Mbunge huyo amehoji serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la vitunguu saumu nje ya nchi.

Akijibu swali hilo, Mgumba amesema vitunguu hivyo vinavyozalishwa nchini hutumika ndani ya nchi na vilevile huuzwa nje ya nchi vikiwa ghafi.

Amesema katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya uhakika kwa mazao ya kilimo ikiwemo vitunguu swaumu, serikali inakamilisha upatikanaji wa Simbomilia na kiwango cha ubora wa bidhaa zinazotokana na vitunguu saumu kutoka Shirika la Viwango Tanzania(TBS).

Aidha amesema wizara imeanzisha kitengo cha masoko chenye jukumu la kutafuta mahitaji ya masoko ya wakulima ndani na nje ya nchi.

Ameeleza serikali kupitia SIDO ilivijengea uwezo vikundi vya wakulima katika bonde la Bashay na kuwawezesha kusindika vitunguu saumu katika bidhaa mbalimbali zikiwemo mafuta na unga.

Mgumba amesema wakulima na wasindikaji wa vitunguu saumu wa Mbulu huwezeshwa kushiriki maonyesho ya kimataifa ya biashara ya Dar es salaam kila mwaka ili kutangaza na kutafuta masoko ya vitunguu saumu.

Habari Kubwa