Serikali kuendelea kupanua Bandari ya Mtwara

29Oct 2019
Mary Geofrey
MTWARA
Nipashe
Serikali kuendelea kupanua Bandari ya Mtwara

SERIKALI inaendelea kupanua Bandari ya Mtwara kwa kujenga gati nne za kisasa kwa ajili ya kuhudumia shehena ya gesi, mafuta na mazao ya Kilimo katika ukanda wa maendeleo wa Mtwara unaojumuisha mikoa ya Kusini na nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Juma Kijavara.

Mradi huo ukikamilika utaiwezesha bandari ya Mtwara kuhudumia shehena zaidi ya tani milioni moja kwa mwaka.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Juma Kijavara, ndiye aliyeyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo leo kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Amesema, awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo ni ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 lenye uwezo wa kuhudumia shehena mchanganyiko unaogharimu Sh. bilioni 137.

Amesema Mamlaka ya Bandari (TPA), iliingia mkataba na Mkandarasi ambaye ni muunganiko wa Kampuni za China Railway Construction Engineering Group na China Railway Major Bridge Engineering Group ulioanza Machi 4, 2017 na unaotarajia kukamilika Machi 2020.

"Hadi sasa kazi ya usanifu imekamilika na kazi ya ujenzi inaendelea na imefika asilimia 55," amesema Kijavara.

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

A post shared by Nipashe (@nipashetz) on Oct 29, 2019 at 8:35am PDT

Naye Kaimu Mhandisi wa Bandari hiyo, Norbart Kalembwe, amesema pia wanaendelea na mradi wa ujenzi wa mita ya kupima mafuta unaitekelezwa chini ya Ofisi ya Rais.

Amesema mradi huo unafanywa na Mkandarasi Endress+Hauser ya nchi ya Uswizi akishirikiana na Kampuni ya Kizalendo ya BQ Constractor kwa ujenzi wa mita za kupima mafuta za Mtwara, Dar es Salaaam na Tanga kwa thamani ya Euro milioni 17.

Amesema kwa Mtwara mradi utahusisha ujenzi wa mitambo miwili pamoja chumba cha usimamizi kwa ajili ya kupima mafuta ya Diseli na Petroli.

Amesema mradi huo ulianza Machi mwaka huu ambao utatekelezwa kwa miezi 15 na unatarajiwa kukamilika Mei mwakani.

"Mradi ukikamilika utakuwa umeiwezesha bandari kutekeleza maelekezo ya Serikali na itakuwa na uwezo wa kupima mafuta halisi yanayopita katika bandari hii," amesema Kalembwe.

Kadhalika amesema wanatekeleza mradi wa ujenzi wa sehemu ya kuhifadhia makasha matupu pamoja na sehemu ya kupanga mzigo kwa msimu wa korosho na ukarabati wa ghala namba tatu.

Amesema mradi huo unafanywa na Mkandarasi Kings Builders akishirikiana na Pioneer Builders na ujenzi ulianza Mei 16, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Mei 17 mwakani kwa thamani ya Sh. milioni 3.297.

"Mradi huu ukikamilika utaiwezesha bandari kuhifadhi shehena kubwa ya makasha kwa wakati mmoja na pia kuwa na hifadhi ya mizigo kwa usalama katika maghala yake," amesema Kalembwe.

Kwa sasa bandari ya Mtwara inahudumia tani 400,000 na miradi hiyo itakapokamilika itaweza kuhudumia tani milioni moja kwa mwaka.

Habari Kubwa