Serikali kujenga Daraja la Jangwani

15Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali kujenga Daraja la Jangwani

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge amesema Serikali itajenga Daraja la Jangwani na kuboresha Mto Msimbazi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Aboubakar Kunenge.

Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 15,2020 Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari. Amesema ile changamoto ikinyesha mvua eneo la Jangwani halipitiki litapatiwa majibu hivi karibuni na kwamba eneo la DAWASA Tegeta na maeneo jirani kutajengwa mifereji ya chini kupeleka maji Baharini.

RC Kunenge amewataka TARURA, TANROAD, DAWASA, REA na TANESCO kuhakikisha wanaendelea kukarabati na kurejesha miundombinu yote iliyoathiriwa na mvua ili huduma ziweze kurejea kama awali.

Amewataka wananchi kuchukuwa tahadhari dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuhakikisha wanafuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ili kujikinga na athari za mafuriko.

"Oktoba 13, Jiji letu lilipata mvua kubwa na kuleta athari ikiwemo vifo 12, nyumba 800 zimeingiliwa na maji, nyumba 107 zimechukuliwa na maji, na Wananchi 480 wamekosa mahali pa kukaa, maeneo yaliyoathirika ni Kisutu,Tupendane,Barafu, Kisiwani nk" amesema RC Kunenge

Hata hivyo RC Kunenge ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutupa takataka kwenye mito na mifereji kwakuwa ndio chanzo cha mitaro kuziba na kusababisha mafuriko.

Habari Kubwa