Serikali kuongeza udhibiti ujio homa mafua ya ndege

03Sep 2017
Renatha Msungu
Nipashe Jumapili
Serikali kuongeza udhibiti ujio homa mafua ya ndege

SERIKALI imejipanga kuimarisha ulinzi katika mipaka yake ili kuendelea kudhibiti magonjwa mbalimbali ya wanyama ukiwamo wa mafua ya ndege ambao ni tishio kwa ukuaji wa sekta hiyo.

Katika mikakati yake ya kudhibiti mafua ya ndege tangu mwaka 2006, serikali iliamua kuzuia uingizwaji wa nyama ya kuku kutoka nchi jirani ili kuepukana na tishio kwa wanyama wengine na binadamu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa viongozi wa Bodi ya Nyama wa mikoa mbalimbali nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Abdul Hayghaimo, alisema lengo la mkutano huo ni kuwajengea uwezo maofisa wanaofanya kazi mipakani ili waweze kudhibiti uingizaji kupitia njia za panya wa bidhaa zitokanazo na mifugo.

Hayghaimo alisema lengo lao ni kuona wanadhibiti njia hizo ambazo siyo halali kutokana na kwamba zinachangia kwa kiasi kikubwa kushusha soko la bidhaa zitokanazo na mifugo nchini.

Alisema kutokana na hilo wao kama bodi ya nyama wanajipanga kudhibiti njia hizo ili waweze kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika sekta ya mifugo.

Aidha, alisema moja ya mikakati ambayo walijiwekea ni pamoja na kutumia Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kuwekea mikakati ya kila mmoja kutakiwa kutopokea mifugo au nyama ambazo hazijaingia kihalali.

“Tumejipanga kutumia njia hiyo katika umoja wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lengo ni kuona tunafanikiwa kudhibiti uhalifu mipakani,” alisema Hayghaimo.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika mipaka 12 inayowazunguka, alisema wanakabiliwa na upungufu wa wafanyakazi.

Alisema katika kila mpaka wanahitajika wafanyakazi wanne, lakini kwa sasa kila kituo kina mfanyakazi mmoja, hivyo hawatoshi kudhibiti njia za panya za kuingiza na kutoa mifugo.

Aidha, alisema tangu mwaka 2006, wamekuwa wakizuia nyama ya kuku kutoka nje ya nchi kuingia nchini kwa sababu ya kuhofia ujio wa homa ya mafua ya ndege iliyowahi kuzikumba nchi za Brazil na Marekani.

Msajili wa Bodi ya Maziwa, Nelson Kiongozi, alisema wana mpango wa kuanzisha viwanda vidogo vya kufungashia  ili biashara za Watanzania ziwe na mvuto zaidi katika masoko.

Habari Kubwa