Serikali kutoa motisha kwa walimu wanaofaulisha 

20Apr 2019
Ibrahim Joseph
KONDOA
Nipashe
Serikali kutoa motisha kwa walimu wanaofaulisha 

SERIKALI imesema itatoa motisha kwa walimu wa shule zake ambazo wanafunzi watafanya vizuri katika taaluma hususani kwenye ufaulu wa mitihani ya kitaifa.

 Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk. Tixon Nzunda, wakati akifunga mafunzo endelevu kwa maofisa elimu kata wa mikoa ya Dodoma na Singida yaliyofanyika wilayani Kondoa.

Dk. Nzunda alisema serikali itatoa motisha kwa walimu ambao wanafunzi wao watafanya vizuri katika taaluma hasa kwenye ufaulu mzuri kwenye mitihani ya kitaifa.

"Motisha itatolewa kwa walimu ambao wanafunzi wao watafanya vizuri katika taaluma, hususani ufaulu mzuri katika mitihani ya taifa.

Dk. Nzunda aliwataka walimu kote nchini kufanya kazi kwa bidii ili kuwawezesha wanafunzi wanaosoma kwenye shule zao kufaulu kwa kiwango cha juu.

Aliwataka maofisa elimu kata kufanya ufuatiliaji wa karibu na kuhakikisha walimu wakuu wa shule husika wanasimamia taaluma kwa bidii.

Aidha, alisema serikali imekubali kutengeneza mkataba wa utendaji kazi kwa kila mwalimu mbali na mfumo wa Opras.

Alisema kila mwalimu anatakiwa kuwa na maandalizi timilifu muda wote awapo shuleni mfano azimio la kazi , andalio la somo na analofundisha pamoja na mpango kazi wa kuongeza ufaulu kwenye somo analofundisha kwa muhula mzima wa masomo.

Alisema mwalimu atapimwa kutokana na idadi ya vipindi kwa muhula mzima wa masomo hali itakayosaidia kuondoa uzembe kazini.

Alisema kipimo kingine cha mwalimu ni kuongeza ufaulu katika somo analofundisha kupitia majaribio ya kitaifa ya darasa la kwanza na la pili, katika eneo la Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na matokeo ya mitihani ya darasa la nne na saba.

Kwa upande wake, msimamizi mkuu wa mafunzo hayo kutoka Chuo cha Maendeleo ya Elimu Bagamoyo (ADEM), Lucas Mzelela, alisema mafunzo hayo yanalenga kuboresha kiwango cha elimu nchini.

Mzelela alisema baada ya mafunzo, maofisa elimu kata kwa kushirikiana na wadhibiti ubora elimu, maofisa elimu taaluma wilaya wataenda kuendesha mafunzo hayo kwa walimu wengine katika maeneo yao.

Aidha, alisema chuo hicho kimepewa jukumu la kuendesha mafunzo hayo nchi nzima na serikali kuhakikisha kuwa watoto wote wanajua kusoma, kuhesabu na kuandika katika kiwango.

Habari Kubwa