Serikali kuwasaka walioficha sukari

26Feb 2016
Na Waandishi Wetu
Dar
Nipashe
Serikali kuwasaka walioficha sukari

SERIKALI imesema itawanyang’anya na kuwafutia vibali vya kuuza sukari nchini mawakala, iwapo watabainika kuficha bidhaa hiyo kwa lengo la kutengeneza uhaba.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema wanaotaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kudhibiti mazingira ya kutengeneza uhaba wa sukari nchini baada ya agizo la Rais Dk. John Magufuli, wanawasha moto na kwamba watafanya ukaguzi katika maghala ili kuwabaini.

Alhamisi iliyopita, Rais Magufuli alitangaza kusitisha kutolewa kwa vibali vya uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi ili kulinda na kuimarisha viwanda vya ndani, lakini baada ya agizo hilo, mapema wiki hii bei ya bidhaa hiyo ilipanda kutoka Sh. 2,000 na kuuzwa Sh. 2, 200 hadi 2,500.

Baadhi ya wafanyabiashara walidai hali hiyo imetoka na bei ya mfuko wa kilo 50 katika maduka ya jumla kwa sasa kuuzwa kati ya Sh. 92,000 hadi Sh. 95,000 wakati awali walikuwa wakinunua Sh. 82,000.

Waziri Mwijage alisema amemuagiza Mkurugenzi wa Leseni ambaye ni ngazi ya halmashauri na wizara kuwaandikia barua mawakala wote wa sukari nchini, kuwataadharisha na hatua zozote za kutaka kuficha sukari na jinsi ambavyo serikali haitalinyamazia suala hilo.

“Sukari siyo sindano, atakayeficha sukari kwa malengo ya kutaka kutengeneza uhaba ili bei ipande, anachezea moto na utamuunguza, tunafanya ukaguzi katika 'magodauni' (maghala) yaliyopo, watambue tutawafungia tuone magodauni watayatumia kuhifadhia nini,” alisema.

Alisema hakutakuwa na mchezo katika hilo kwa kuwa serikali imedhamiria kuimarisha viwanda vya ndani na kuwezesha miwa ya wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri.

Waziri Kaijage alisema tangu kutolewa kwa agizo la Rais, wawekezaji wameanza kujitokeza na kutaka kujenga viwanda vya sukari kwa kuwa wana uhakika wa soko, na kwamba tajiri Dangote ameomba kupewa eneo na kwamba Mkoa wa Kigoma umetenga ekari 100,000 ambazo mwekezaji kutoka India amepelekwa kuonyeshwa eneo husika na maeneo ya Babati na Morogoro kuna wawekezaji wadogo wanatarajia kujenga viwanda.

Alisema sekta ya sukari ni yenye kutegemeana tangu uzalishaji na lolote linalofanyika nje ya utaratibu linaathiri mfumo mzima, jambo ambalo serikali haitakubali.

“Wenye viwanda watapewa maelekezo waeleze wanalima kiasi gani na kuzalisha sukari kiasi gani, namna watakavyowasaidia wakulima wa miwa na kuwalipa bei nzuri kwa miwa yao, gharama za uzalishaji wa kilo moja ya sukari ndiyo itaonyesha bei inayopaswa kuuzwa kwenye maduka ya kawaida,” alisema.

Waziri huyo alisema mahitaji yanayominywa kwa sasa ni tani 590 huku uwezo wa viwanda kuzalisha sukari ukiwa tani 320,000, na kwamba tani 700 ambazo ndiyo uhaba zitapatikana kwa viwanda kuongeza uzalishaji na hivyo kutokuwa na haja ya kuagiza sukari nje.

Wakati bei ya sukari ikipanda, wenye viwanda wamesema bidhaa hiyo ipo ya kutosha.

Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Tawala wa Kiwanda cha Sukari ya Moshi (TPC), Jaffar Ally, alisema kwa upande wao wana zaidi ya tani 19,000 ambazo zipo kiwandani.

“Si kweli kama kuna uhaba wa sukari, kiwanda chetu kwa sasa kina tani zaidi ya 19,000, hawa wafanyabiashara wanataka kujiingizia fedha, kiwandani tunauza kwa bei jumla ya Sh. 1,400 ambayo haijabadilika kutoka awali,” alisema na kuongeza:

“Inashangaza mtu ambaye hazalishi, hana kiwanda halafu anapata faida kubwa kuliko sisi...kama wanauza kwa bei ya Sh. 2,200 hadi 2,500 wanapata faida ya Sh. 1,000,” alisema.

Msemaji wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa kilichopo Morogoro, Hamad Yahaya, alisema hakuna tatizo la upungufu wa sukari kwani kiwandani kwake kuna zaidi ya tani 40,000 ambazo wana uwezo wa kuzisambaza nchi nzima.

Alibainisha sababu ya kupandishwa sukari na wafanyabiashara hao ni kutokana na kukwepa ushuru kwa sukari iliyokuwa inaagizwa kutoka nje.

“Hawa walikuwa wakijipangia bei zao wanazotaka sokoni kwa kuwa walikuwa wanakwepa kodi, wameona wamebanwa na serikali wamepandisha bei,” alisema.

Aliongeza: “Kupandishwa kwa sukari na kufikia Sh. 2,200 hiyo ni bei halisi kwani kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano sukari inauzwa sh. 2,000,” alisema.

Hata hivyo, alisema kauli ya Rais Magufuli kuzuia kutolewa kwa vibali wanataka kuitumia ionekane kuna ukosefu wa sukari, jambo ambalo siyo la kweli.

Imeandaliwa na Salome Kitomari, Romana Mallya na Beatrice Shayo.

Habari Kubwa