Serikali kuzibana tiba asili, mbadala

05Mar 2016
Efracia Massawe
Nipashe
Serikali kuzibana tiba asili, mbadala

SERIKALI imesema itahakikisha inadhibiti tiba asilia na mbadala kwa kuchukua sampuli za mimea kutoka kwenye vitalu vya watabibu wa tiba asili na kuifanyia vipimo kuangalia matumizi ya miti kwa kila mmea.

Naibu Waziri wa Afya, Dk.Hamis Kigwangalla

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam, Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Profesa Samwel Manyele, alisema nia ya serikali ni kuwabana watabibu hao.

Alisema kabla tiba hiyo haijatumika, inatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kemikali zinazotumika kama zinakidhi matakwa ya malaji.

“Tumejadiliana na Wizara ya Afya, tukawashirikisha baadhi ya viongozi wa vyama vya tiba asili na mbadala, tukawapa mawazo ya kitaalamu kuhusu dawa za asili na kemikali zilizoko,” alisema Manyele.

Aidha, wakala huo umesema utawakutanisha viongozi wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), Jukwaa la Tiba Asili Tanzania, Baraza la Tiba Asili na Mbadala na Wizara ya Afya kujadili suala hilo.

“Tutaweka tiba asili katika 'Databese' ya taifa ambapo watanufaika pamoja na kubaini ugonjwa wanaotibu kupitia mimea hiyo,” alisema.

Alisema kupitia mkutano huo, matabibu wa tiba asili watapata uelewa wa sayansi ya miti shamba na njia ya kuwasilisha sampuli na kuzijua kemikali zilizo hatarishi katika mimea.

Tangu mwaka 1969 jukumu la kupima tiba asili ni la mkemia mkuu wa serikali, alisema Profesa Manyele, lakini baadaye wakala huo ulisuasua.

Alisema serikali itarudisha msimamo wake wa awali huo ili kudhibiti kemikali zinazoingia katika tiba hiyo.

Habari Kubwa