Serikali Mwanza kuwezesha miradi ya ufugaji

15Sep 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
Serikali Mwanza kuwezesha miradi ya ufugaji

SERIKALI mkoani Mwanza imejipanga kuwezesha miradi ya ufugaji wa samaki kwa vizimba ndani ya Ziwa Victoria itakayogharimu sh.bilioni 1.9 ili kuwasaidia vijana na kada nyingine kujiajiri na kunufaika na uchumi wa bluu.

Hayo yalielezwa na Peter Masumbuko,  wakati akiwasilisha taarifa ya utafiti wa mradi huo, kwenye mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Mwanza lililokutaka kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta binafsi hasa wafanyabiashara.

Alisema mradi huo wa kuanzisha vikundi vya ufugaji wa samaki aina ya sato wa jinsia moja kwa vizimba utapunguza changamoto ya ajira kwa vijana na kuwanufaika kiuchumi na kimazingira.

Kwa mujibu wa Masumbuko, kila wilaya itatakiwa kuanzisha vikundi vitano vinavyotambuliwa kuanzia ngazi ya chini ambavyo vitawezeshwa mitaji itakayovifanya vinufaike na uchumi wa bluu unatokana na maji.

Aidha akitoa uzoefu wake kwenye eneo la uwekezaji wa ufugaji wa samaki kwa vizimba,mkuu wa zamani wa mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro, Mecky Sadiki,alisema licha ya Tanzania kumiliki asilimia 53 ya Ziwa Victoria bado haijanufaika na umiliki huo kutokana na migongano ya sheria kulinganisha na nchi za Kenya na Uganda.

Alisema ufugaji wa samaki kwa vizimba unalipa na kushauri watu wasiogopeshwe wala kukatishwa tama na gharama za uwekezaji, na kuhimiza uanzishaji wa vizimba vingi kwani soko la uhakika lipo likiwemo la malighafi ya kutengeneza chakula cha samaki.

“Tunajichelewesha sisi wenyewe, hakuna mazingira yataharibiwa kwa ufugaji wa vizimba,kwa kutumia teknolojia hii wavuvi haramu wataondoka wenyewe na huo ndio mbadala wa kumaliza uvuvi haramu,tatizo ni tozo kubwa mfano Ukerewe kilo moja ya samaki inatozwa ushuru wa sh.300,”alisema Sadiki.

Mkurugenzi wa Zara Solar,Mohamed Parpia, alishauri kuwa ipo kampuni moja ya nchini Uhalonzi inawezesha mikopo ya Dola 300 za Marekani kwa wafugaji wa samaki, lakini inahofia fedha kuliwa hivyo masharti lazima waingizwe kwenye uendeshaji.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akifungua baraza hilo alisema, uchumi wa bluu bado hatujafanya kitu cha kuukamata ilhali malighafi na ziwa tunalo,watu wapo wakiwemo wasomi wa kada na taaluma mbalimbali.

Pia alishangaa chakula cha samaki kuagizwa kutoka nje ya nchi na kuhoji ni wapi tumekwama na kushauri wasomi waliopo kuangalia mazingira ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Mwanza lengo likiwa ni tunufaika na kuziona fursa zitakazoleta mapinduzi ya kiuchumi.

“Mwanza kuna fursa kubwa ya kiuchumi, kwenye utalii na maji, hivyo lazima tuwe na maono yenye nguvu yatakayosababisha tusilale,yatuletee mapinduzi ya kiuchumi,tutoke tulipo na tukimbie,”alisema  Mhandisi Gabriel