Serikali sasa yapiga marufuku mtoto kusafirishwa bila kibali

12Aug 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Serikali sasa yapiga marufuku mtoto kusafirishwa bila kibali

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama nchini, kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18, anayesafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine anakuwa na kibali cha mzazi na kile cha kiongozi wa serikali za mitaa.

Pia, amemwagiza katibu mkuu wa Wizara yake, kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje, ili kuwabaini na kuwarejesha nchini Watanzania wote waliopo nje ya nchi ambao wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kutumikishwa.

Simbachawene aliyasema hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akifungua maadhimisho ya kitaifa kupinga biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Alisema hivi sasa nchini hali ni mbaya hasa katika maeneo ya miji mikubwa ambapo biashara ya kusafirisha watu imeshamiri hasa kwa wanawake na watoto wa kike.

Alisema kutokana na hali hiyo, vyombo vya ulinzi katika Wizara yake vinatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kukabiliana na biashara hiyo haramu ya kusafirisha binadamu.

Alisema vyombo vya ulinzi vinatakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyozoeleka bali vinatakiwa kutimiza majukumu yao kwa vitendo.

“Biashara hii hata hapa tukisema tutoke twende kwenye mabasi barabarani tukafanye ukaguzi kwenye mabasi lazima tutawakuta watoto watatu hadi wanne, ambao wanasafirishwa bila wao kujua kule wanakokwenda wanakwenda kufanya nini,”alisema Simbachawene.

Waziri huyo alisema kutokana na hali hiyo, vyombo vya ulinzi vinatakiwa kuacha kufanya kazi kwa nadharia bali viendeshe misako mikali katika magari mbalimbali ili kukomesha biashara hiyo haramu.

Vile vile, alisema pamekuwapo na watu ambao ni maarufu kwa kukusanya watoto kutoka katika mikoa mbalimbali na kwenda kuwauza kwa watu wanaohitaji wasichana wa kazi.

Aliwaonya Watanzania kutotumia kigezo cha umasikini na ukosefu wa ajira nchini kama kichocheo cha kuruhusu kirahisi vijana na mabinti kwenda nje ya nchi kwa sababu ya kutafuta kazi, ambapo alisema ni vyema kutumia fursa na rasilimali zilizopo kujikwamua.

Alisema, wengi husafirishwa kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi, baada ya kufika huko wanajikuta wanaishia kutumikishwa katika biashara ya ukahaba hususani katika nchi za India, Thailand, China, Indonesia na Malasya.

Alisema kuwa, wengine wanatumikishwa kwa kazi za ndani katika nchi za Oman na baadhi ya nchi nyingine za uarabuni ikiwemo Iraq.

Alieleza kuwa, wahanga wengi wanaosafirishwa nje ya nchi wanatokea jijini Dar es Salaam, Tanga na Dodoma (Hususani Wilaya ya Kondoa) na wachache ni kutoka mikoa mingine na waathirika wakubwa ni wanawake kuanzia umri wa miaka 16 hadi 26.

Mkuu wa shirika la kimataifa linalojihusisha na masuala ya uhamaji (IOM), Dk. Qasim Sufi, alisema, huu ni mwaka wa 20, wanafanya maadhimisho ya kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya kuzuia na kupambana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, Adatus Magere, alisema biashara hiyo ina mtandao mkubwa kimataifa na kitaifa.

Alisema kuwa biashara hiyo inahusisha magenge ya kimataifa yanayojihusisha na uharifu, na wakati mwingine inahusishwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Habari Kubwa