Serikali, Total kufanya utafiti wa mafuta

15May 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali, Total kufanya utafiti wa mafuta

SERIKALI kwa kushirikiana na Kampuni ya mafuta ya Total inatarajia kufanya utafiti wa mafuta nchini na kiwango kitakachogundulika kuwezesha kuubadili uchumi wa nchi.

Makamu Rais wa Kampuni ya mafuta ya Total Kanda ya Afrika, Kaskazini, Kati na Afrika Mashariki, Jean Philippe Torres (kushoto), akibadilishana mawazo na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania, Tarik Moufaddal, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya kampuni hiyo. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Waziri wa Nishati, Titus Kalemani, alisema hayo wakati wa hafla ya kuwapongeza wafanyakazi na wadau wa Total Tanzania, katika Maadhimisho Total ya miaka 50 nchini.

 

Waziri Kalemani alisema utafiti umethibitisha, kila mahali ilipogunduliwa gesi asili, chini yake kuna mafuta, hivyo serikali imeanza mazungumzo na kampuni ya Total Tanzania, ili kufanya utafiti wa mafuta na kuwataka Watanzania kuipatia ushirikiano kampuni hiyo.

Aliipongeza kampuni hiyo kwa kazi zake kubwa sita inazozifanya nchini Tanzania, ikiongozwa na kuuza mafuta, vilanishi vyenye ubora, kujenga bomba la mafuta la Uganda, kusambaza nishati mbadala ya nishati jua, kutoa ajira za kudumu na za muda kwa Watanzania na kuchangia huduma kwa jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania, Tarik Moufaddal, alisema katika kipindi cha miaka 50, kampuni hiyo imefanya makubwa na kuongoza kwa wingi wa vituo vya mafuta, kuuza mafuta yanayoongoza kwa ubora na  vilanishi vyenye ubora na kutoa huduma za jamii.

 

Sherehe za Maadhimisho hayo, zilizinduliwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye pia aliwakabidhi zawadi mbalimbali wafanyakazi wa muda mrefu wa kampuni hiyo na wadau wake.

Habari Kubwa