Serikali yaahidi jeshi la kisasa

17May 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Serikali yaahidi jeshi la kisasa

SERIKALI imesema mwaka ujao wa fedha, itapatia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vifaa na zana bora za kisasa kwa lengo la kuwa na jeshi la kisasa.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussen Mwinyi.

Vievile, imesema itatoa mafunzo kwa wanajeshi ili kuliongeza uwezo na weledi wa kiutendaji, kiulinzi na kivita.

Akiwasilisha hotuba bungeni jijini Dodoma jana kuhusu makadirio ya bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussen Mwinyi, alisema wizara hiyo pia imepanga kutekeleza vipaumbele 12.

Alivitaja kuwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kikazi kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma stahiki na mahitaji ya msingi kwa wanajeshi na watumishi wa umma.

Alisema wizara yake pia itawapatia vijana wa Tanzania mafunzo ya ukakamavu, umoja wa kitaifa, uzalendo na stadi za kazi.

Alisema wizara pia itaendeleza utafiti na uhawirishaji wa teknolojia kwa kuimarisha na kuanzisha viwanda kwa madhumuni ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kiraia huku ikiimarisha ushirikiano na jumuiya za kimataifa, kikanda na nchi moja moja katika nyanja za kijeshi na kiulinzi.

Alisema mpango mwingine wa wizara mwakani ni kupima, kuthamini na kulipa fidia ya ardhi katika maeneo yaliyotwaliwa kwa ajili ya matumizi ya jeshi.

Dk. Mwinyi aliongeza kuwa jeshi litaendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura pale inapohitajika,

"Wizara pia italipa stahili mbalimbali za maofisa, askari, vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa na watumishi wa umma, kukamilisha Sera ya Ulinzi wa Taifa, Mwongozo wa Viwanda Jeshini na Mpango wa Maendeleo wa Miaka 10 yaani 2018/29-2027/28 wa kuliimarisha Shirika la Nyumba," alisema.

Aliongeza kuwa hali ya usalama wa mipaka ya Tanzania kuwa ni nzuri licha ya kuwapo tishio kutoka kwenye vikundi vya kigaidi katika baadhi ya nchi jirani.

Waziri huyo alisema wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali, kubwa ikiwa ni ufinyu wa bajeti, akibainisha kuwa Sh. trilioni 1.9 ilizoidhinishiwa na Bunge kwa ajili ya mwaka huu wa fedha, hazikidhi mahitaji halisi.

Ili kutekeleza majukumu yake, Dk, Mwinyi aliliomba Bunge kuidhinisha Sh. trilioni 1.85 kwa ajili ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Kati yake, Sh. trilioni 1.72 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 128 ni za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Habari Kubwa