Serikali yaajiri walimu 4,549 kati ya 91,108 waliotuma maombi

27Apr 2019
Mary Geofrey
Dar es salaam
Nipashe
Serikali yaajiri walimu 4,549 kati ya 91,108 waliotuma maombi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo, amesema jumla ya walimu 4,549 wamepangiwa kufundisha katika shule za Msingi na Sekondari katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri wa tamisemi Suleiman jafo.

Jafo amesema Tamisemi ilipata kibali cha kuajiri jumla ya walimu 4, 549 na kibali hicho kilikuwa kwa ajili ya walimu wa shule hizo na hasa katika maeneo yaliyokuwa na upungufu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Jafo amesema jumla ya waombaji 91,108 walojitokeza kutuma maombi ya nafasi mbalimbali zilizotangazwa na kati ya hao maombi 43,770 sawa na asilimia 48.04 ya waombaji wote walikuwa na viambatisho vyote vilivyohitajika.

Ameongeza na jumla ya waombaji 47,338 sawa na asilimia 51.96 maombi yao hayakuwa na vigezo ikiwa ni pamoja na kukosa viambatisho muhimu vilivyohitajika.

“Kutokana na mahitaji makubwa ya walimu katika shule za msingi na walimu wa shule za msingi wa masomo ya sayansi(Fizikia,Kemia na Bailojia) na hisabati .Ofisi ya TAMISEMI imefanya uchambuzi na kutoa kipaumbele katika ajira ya walimu wa kada za walimu daraja la tatu A(cheti)kwa ajili ya kufundisha shule za msingi.

“Walimu daraja la tatu B (Stashahada) wa masomo ya sayansi kwa ajili ya kufundisha shule za sekondari kidato cha kwanza hadi kidato cha nne.Walimu daraja la tatu C wa masomo ya sayansi kwa ajili ya kufundisha katika shule za sekondari za kidato cha tano na sita,"alisema Jafo.

Ameeleza kuwa walimu daraja la tatu C (Shahada) wa masomo ya elimu maalum ,biashara, uchumi, kilimo na maarifa ya nyumbani kwa ajili ya kufundisha shule za sekondari.

Amesema mchakato wa kupitia maombi ulijumuisha uhakiki wa uhalali wa vyeti vy elimu na taaluma vya waombaji na ukamilifu wa nyaraka zilizohitajika," amesema Jafo.

Amefafanua anatumia nafasi hiyo kuwataarifu waombaji wote wa masomo ya Sana, Sayansi na masomo mengine ambao walitimiza vigezo na hawakufanikiwa kupata nafasi katika kipindi hiki kuwa maombi yao yote yamechambuliwa na yamehifadhiwa kwenye kanzidata yao na kuwa fursa za ajira zitakapojitokeza utaratibu wa ajira utatolewa.

Kuhusu walimu waliopata ajira ambao ni hao 4,549 wamepangiwa moja kwa moja na kati ya hao jumla ya walimu 3,059 sawa na asilimia 67.25 wamepangiwa kufundisha shule za msingi na walimu 1,490 sawa na asilimia 32.75 wamepangwa kufundisha shule za sekondari.

Amewataka walimu wote waliopata ajira wanatakiwa kuripoti kwa wakurugenzi wa halmashauri zilipo shule walizopangwa kwa ajili ya uhakiki wa vyeti halisi vya elimu na taaluma,kujaza mikata ya ajira na taratibu nyingine za kiutumishi na kisha kuripoti katika shule walizopangiwa.

Amesema walimu wote waliopata ajira wanatakiwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi kuanzia Mei 7,2019 hadi Mei 21,2019 na walimu wapya ambao hawataripoti katika vituo vyao vya kazi ifikapo Mei 21,2019 nafasi zao zitajazwa mara moja bila kuwataarifu kwa kuwapanga walimu wenye sifa ambao hawakupangwa katika awamu hii.

“Aidha, wakurugenzi wa halmashauri wasibadilishe vituo vya kazi vya walimu hao bila kibali maalum cha Katibu Mkuu Tamisemi .Mwajiriwa atakayeripoti na kuchukua posho ya kujikimu kisha akaondoka katika kituo chake cha kazi alichopangiwa atachukuliwa hatua kali za kisheria," amesema Jafo.

Pia ameomba wakurugenzi wote wa halmashauri zilizopangiwa walimu wa ajira mpya kuwapokea walimu hao na kukamilisha taratibu za ajira kwa kuzingatia sheria ,kanuni ,taratibu na miongozo inayosimamia utumishi wa umma.

Habari Kubwa