Serikali yaanika mkakati soko la chai

15Jan 2019
George Tarimo
Mufindi
Nipashe
Serikali yaanika mkakati soko la chai

WIZARA ya Kilimo imesema imeweka mkakati kabambe wa kuinua zao la chai nchini kwa kuanzisha soko la uhakika.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo,  Inocent Bashungwa, wakati akizungumza  na wananchi na wanachama wa chama cha ushirika cha wakulima wa chai katika kijiji cha Mkonge Kata ya Luhanga Tarafa ya Ifwagi,  alipotembelea  wakulima wadogo na wakubwa wa chai wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Bashungwa akiwa katika kijiji hicho alieleza namna wizara ilivyojiwekea mkakati wa kuinua zao la chai nchini, ikiwa na  lengo la kumnufaisha mkulima ili kulifikisha taifa katika uchumi wa kati kwa kuwa zaidi ya asilimia 65.5 nchini ni wakulima, hivyo ni lazima kuunganisha kilimo na viwanda ili kufikia lengo hilo.

“Ni wakati sasa wa kuona zao la chai linamnufaisha mkulima, nimeshawaelekeza Bodi ya Chai Tanzania haraka iwezekanavyo tuleta ule mkakati wa kitaifa wa kufufua zao la chai nchini na tutoke kwenye uzalishaji wa tani 34,000 za sasa na angalau kufikia tani 40,000 ili tuweze kuwafikia wenzetu wa Kenya,” alisema Bashungwa.

Bashungwa alisisitiza kwamba ni lazima mkulima aone  zao hilo ni la kimkakati na linamuondoa kwenye umaskini.  

“Uzalishaji wa chai kwenye upande wa masoko tayari tumeshaagiza Bodi ya Chai kufikia Mei mwaka huu mkakati wa kuanzisha soko la chai jijini Dar es Salaam unakamilika na kuhakikisha chai inauzwa nchini ili mwaka wa fedha wa 2019/2020 unapoanza Julai tunakuwa na mnada ili gharama za usafirishaji chai nje zinapungua, na faida ile ije kumsaidia mkulima,” alisema.

Bodi ya Chai kupitia kwa mjumbe wake Dk. Emmanuel Simbua, alieleza namna mchakato unavyofanyika wa upangaji bei na kuahidi kubadilisha viwango vya bei elekezi ya ununuzi wa chai kutoka kwa wakulima mwaka huu 2019 kwa kuwashirikisha wadau wote.

Alisema kutokana na changamoto mbalimbali za wakulima kabla ya Februari  mwaka huu kitafanyika kikao cha wadau wa chai nchini wilayani Mufindi kwa sababu ndipo asilimia takribani 70 ya uzalishaji wa chai  nchini unafanywa pamoja na Wilaya ya Njombe, lakini changamoto nyingi za wakulima wa zao hilo zitapatiwa ufumbuzi.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William, alisema serikali imejitahidi kutafuta wafadhili na wadau mbalimbali ambapo wa Mufindi, Cosato Chumi, alikuja na wataalamu kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Mijini (TARURA) kutoka makao makuu Dodoma kwa ajili ya kushughulikia suala la barabara ya kilomita 40 kutoka Sawala hadi Lulanda ikiwa ni moja ya kupunguza changamoto ya miundombinu ya barabara katika mashamba ya chai ili kuzisafirisha kwa urahisi.

Katibu wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Chai Mkonge, Venusto Chang’a, alieleza kwamba changamoto nyingine ni mkulima kutoshiriki katika mnyororo wa thamani katika zao la chai kwa kuishia kuuza majani mabichi pekee na bei kubwa ya pembejeo inayopatikana bila ruzuku ya serikali.

Akijibu changamoto ya bei Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania, Theophord Ndunguru, alikiri changamoto hiyo na kusema tatizo hilo linatokana na mnada wa soko kuwa Mombasa nchini Kenya, hivyo wao kujipendelea pamoja na ubora wa chai, hivyo serikali imeshaanza mkakati wa kuanzisha mnada wake jijini Dar es Salaam ili kusaidia bei kupanda utakamilika Mei.

Habari Kubwa