Serikali yadhamiria kuanzisha kiwanda cha simu janja

16May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Serikali yadhamiria kuanzisha kiwanda cha simu janja

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu, amesema serikali imedhamiria kuanzisha kiwanda cha kuzalisha simu janja (smart phones) ili kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wote nchini wanapata huduma za mtandao ifikapo mwaka 2025.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu.

Dk. Nungu amesema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea wiki ya ubunifu inayoanza kesho Mei 17 jijini Dar es Salaam na kumalizika Mei 22, 2021.

Amesema uanzishwaji wa kiwanda hicho cha simu utaenda sambamba na upanuzi wa upatikanaji wa mkondo wa Taifa ili kuunganisha maeneo mengi yenye makazi ya watu yasiyofikiwa na kampuni za simu.

Wiki hiyo ya Ubunifu nchini imeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Binadamu (HDIF) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP).

Amesema kauli mbiu ya wiki ya Ubunifu mwaka huu ni Uchumi wa kidijitali stahimilivu na jumuishi, ambapo ili kufikia malengo hayo serikali iliamua kuanzisha Wizara inayoshughulikia masuala ya Tehama ili kila mtu aweze kufikiwa na huduma hizo.

Amesema kuwa, hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza zabuni kwa wadau mbalimbali watakaoweza kuanzisha kiwanda cha kuzalishia simu janja ili simu hizo ziweze kupatikana kwa bei nafuu na kuongeza ajira

Habari Kubwa