Serikali yaelekeza nguvu kwenye sekta ya misitu

30Nov 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yaelekeza nguvu kwenye sekta ya misitu

SERIKALI imeanza kuboresha mazingira  katika sekta ya  misitu ili kuhakikisha inachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi, kuwaongezea wananchi kipato na kuzalisha ajira. 

Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohamed Kilongo, alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili shughuli za uchumi na biashara ziongezeke na kuzalisha ajira.
 
Alisema kama ilivyo kwa sekta nyingine, wanaamini kuwa sekta ya misitu ikiboreshwa zaidi na kuthaminiwa na wafanyabiashara, itakuwa ni mkombozi kwa Watanzania wengi.
 
“Miaka ya nyuma serikali ilianzisha mashamba makubwa ya mitiki ili kuepukana na matumizi makubwa ya mbao ngumu za miti ya asili, na ndiyo maana kwa sasa tumeona kuendeleza nia njema hiyo kwa kuweka mazingira mazuri zaidi katika kuhamasisha matumizi ya miti mingine ikiwamo ya misaji ambayo nayo ina ubora sawa na mbao za mninga na mkongo,”  alisema na kuendelea:
 
“TFS ina mashamba makubwa ya miti ya misaji ambayo kwa mwaka inatoa zaidi ya mita za ujazo 20,000 na tumeanza kuhamasisha watu watumie mbao za miti hiyo, lakini kuhakikisha mbao zake zinaingia kwenye mlolongo wa serikali na kutambulika kama ilivyo kwa mkongo na mninga.”
 
Pantaleo Banzi, Mwenyekiti wa wafanyabiashara za samani wa Keko jijini Dar es Salaam, alisema wamebaini kwamba mbao za misaji licha ya ubora wake zinapatikana kwa urahisi na hivyo kuwashauri watu kuziangalia kwa jicho la tatu.
 
Mwakilishi wa wafanyabiashara wanaosafirisha mbao za misaji nje ya nchi, Malima Mrungu, alisema aina hiyo ya mbao imekuwa na soko kubwa na inapendwa zaidi nje ya Tanzania.

 

Habari Kubwa