Serikali yafuta leseni 200 za uchimbaji

02May 2022
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Serikali yafuta leseni 200 za uchimbaji

SERIKALI imefuta leseni 200 za uchimbaji wa madini ambazo wamiliki wake wameshindwa kuzifanyia utafiti na kuanza uchimbaji, huku taratibu za kufuta zingine 400 zikiendelea.

Waziri wa Madini, Doto Biteko, alitoa takwimu hizo mwishoni mwa wiki bungeni wakati akijibu hoja za wabunge kwenye hitimisho la hoja yake ya kuomba makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2022/23.

Waziri Biteko alisema kuna maeneo wafanyabiashara walipewa leseni za uchimbaji madini lakini hawajafanya lolote kwa miaka mingi kwa mtazamo wa macho.

Waziri Biteko alisema: “Nataka kuwahakikishia kwamba Wizara ya Madini tangu tumeanza kuwapa nguvu wachimbaji wadogo tunapata lawama sana kwamba tunafuta leseni, lakini sisi tunatekeleza maelekezo ya Bunge na viongozi wetu.”
Aliongeza: “Hadi sasa tumeshafuta leseni zaidi ya 200 ambazo ni domant (mfu), zipo nyingine nyingi zaidi ya 400 ambazo process (mchakato) wa kuzifuta unaendelea.

“Process (mchakato) wa kufuta leseni una lawama nyingi, sisi Wizara ya Madini tumekubali kubeba lawama kwa niaba ya wachimbaji wadogo.”

Waziri Biteko alisema kuna wachimbaji madini wenye tabia ya kushika maeneo kwa maana ya udalali, wanategeshea kuona nani anakuja , wengine wanasubiri hadi wachimbaji wadogo waje kuchimba ndipo anajitokeza na kuwaambia hili ni eneo langu na kuanza kuwafukuza.

“Naomba niwaambie wachimbaji wakubwa wa madini wanaotekeleza sheria tutawalinda lakini wale ambao hawatekelezi sheria maeneo yao tutayachukua na kuwapatia wale ambao wanahitaji kufanya uchimbaji,” alisema Waziri Biteko.

Hata hivyo, alisema katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi, 2022, Tume ya Madini imetoa leseni 8,172 za uchimbaji madini ikilinganishwa na leseni 6,314 katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021, sawa na ongezeko la asilimia 17.3.

Alisema leseni hizo zinajumuisha leseni mbili za uchimbaji mkubwa, leseni tano za uchimbaji wa kati, leseni 282 za utafutaji wa madini, leseni 5,937 za uchimbaji mdogo, leseni 49 za uchenjuaji wa madini, leseni mbili za usafishaji wa madini na leseni 1,895 za biashara ya madini.

Aidha, akitaja vipaumbele vya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23, Waziri Biteko alisema wataendelea kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa.

Alisema pia wizara yake itawaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa madini, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini.

Kipaumbele kingine ni kuhamasisha biashara na uwekezaji katika sekta ya madini, kusimamia mfumo wa ukaguzi wa shughuli za migodi, kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.

Habari Kubwa