Serikali yafuta mashamba sita ya Mohammed Enterprises

14Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Korogwe
Nipashe
Serikali yafuta mashamba sita ya Mohammed Enterprises

Serikali imeyafuta mashamba sita yenye ukubwa wa hekari 12, 915.126 ya kampuni ya Mohammed Enterprises yaliyopo korogwe mkoa wa Tanga.

Mohammed Dweji anayedaiwa kuwa mmiliki wa mashamba hayo, picha mtandao

Uamuzi wa kufuta mashamba hayo unafuatia kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na halmashuri ya wilaya ya Korogwe kuyafuta mashamba yasiyoendelezwa kwa muda mrefu na baadaye maombi hayo kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wizara kwa nia ya kufutwa.

Mashamba yaliyofutwa ni yale yaliopo eneo la Mombo, Mabogo pamoja na Kwalukonge.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mashamba hayo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, amesema mashamba yaliyobatilishwa ni kati ya mashamba 14 yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises Mazinde wilayani Korogwe, na kubainisha kuwa uamuzi huo unalenga kujenga nidhamu kwa waliopewa rasilimali za serikali ili kuzingatia masharti ya uwekezaji.

Alisema, mara baada ya halmashauri ya wilaya ya Korogwe kupeleka mapendekezo ya kufutwa mashamba ya Mohammed Enterprises, wizara ya ardhi ilifanya ufuatiliaji juu ya mambo ya halmashauri husika la kutoendelezwa mashamba na baada ya kujiridhisha ikawasilisha maombi hayo kwa rais na kuridhiwa.

Alisema, uamuzi huo wa Rais kuridhia ubatilishaji mashamba sita kati ya 14 yanayomilikiwa na Mohammed Enterprises unalenga kuhakikisha wote waliopewa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wanazingatia masharti na taratibu za uwekezaji.

Hata hivyo, Mabula alisema mashamba ambayo hayajabatilishwa yamewekewa utaratibu kwa nia ya kuyaboresha kwa kuwa baadhi yake yanahitaji maboresho kwa nia ya kufanya vizuri.

Ameitaka halmashauri ya Korogwe kupanga mpango wa matumizi bora ya ardhi katika eneo la mashamba yaliyofutwa na kipaumbele kwa watakaopewa maeneo katika mashamba hayo ni wananchi waliokuwa wakiishi katika mashamba hayo na sehemu itakayobaki atafutwe mwekezaji mwingine kwa kuwa lengo la serikali ni kuwa na uwekezaji wa viwanda.

Aidha, Mabula alimpongeza Mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigela, kwa kufanya kazi nzuri ya kufuatilia na kusimamia maagizo mbalimbali tangu Rais alipoanza kubatilisha mashamba ambayo hayajaendelezwa katika mkoa wa Tanga.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa huo aliwataka wananchi wa Korogwe kutovamia maeneo ya mashamba yaliyobatilishwa hadi hapo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe itakapopanga matumizi bora ya ardhi katika mashamba hayo.

Alisema, ndani ya wiki hii ataitisha mkutano na wataalamu wa sekta ya ardhi katika mkoa huo pamoja na wale wa bodi ya Mkonge kuangalia matumizi ya ardhi iliyobatilishwa kwa wananchi na uwekezaji.