Serikali yafuta uagizaji mbolea kwa zabuni

22Jul 2021
Beatrice Moses
Nipashe
Serikali yafuta uagizaji mbolea kwa zabuni

SERIKALI imefuta utaratibu wa kuagiza mbolea kwa zabuni, baada ya kubaini haiwasaidii wakulima.

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda.

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam na kueleza kwamba kwa sasa wigo wa uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi umefunguliwa kwa wafanyabiashara wenye nia ya kufanya biashara hiyo.

“Tunaamini hatua hii itasaidia mbolea kuingia kwa wingi nchini hivyo wafanyabiashara watakuwa na bei ya ushindani, haimuumizi mkulima, pia tunachoangalia sisi mbolea inayoletwa iwe na viwango vya ubora unaotakiwa,” alisema.

Alisema mfumo wa zabuni haujawasaidia kwa kuwa kampuni nyingi zinazojitokeza lakini yanachukuliwa machache, bei inapangwa ambayo siyo rafiki kwa wakulima.

“Japo hatuna uwezo wa kushusha bei kwenye soko la dunia lakini tunahitaji kuona wafanyabiashara wanasaidia kuwezesha mbolea kupatikana kwa wingi, Serikali inafanya juhudi ikiwamo kupunguza gharama za kulipia maghala ya kuhifadhi,”alisema Prof. Mkenda.

Alibainisha lengo la serikali ni kuwaona wakulima wanapata faida kutokana na kilimo, ndiyo maana haijaweka kodi yoyote kwenye mbolea.

Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Dk. Anselm Moshi, alisema ununuzi wa mahindi ni kati ya Sh.250 hadi 480 ikitofautiana kwenye mikoa husika.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA),  Militon Lupa, alisema wanatarajia kununua tani 165,000 za aina tatu za nafaka kwa msimu wa mwaka 2021/2022 kutoka kwenye mikoa yenye uzalishaji mkubwa, kati ya aina hizo mahindi ni tani 150,000.

Habari Kubwa