Serikali yafuta vipindi vya nyongeza

03Jul 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yafuta vipindi vya nyongeza

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imefuta saa mbili za nyongeza za masomo zilizokuwa zinafundishwa kila siku kwa shule za msingi na sekondari.

Saa hizo ziliongezwa kufidia muda uliopotea kutokana na wanafunzi kuwa nyumbani tangu Machi 18, mwaka huu, kutokana na janga la corona. Shule zilifunguliwa Jumatatu wiki hii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamishina wa Elimu, Lyabwene Mtahabwa, kwa sasa wanafunzi watarejea kwenye utaratibu wa kusoma vipindi nane kwa siku.

Alisema tathmini iliyofanyika ya utekelezaji wa malekezo ya awali ya Wizara, imeridhika kuwa kuongezeka kwa saa mbili kila siku ni vigumu kutekeleza.

“Hii ni kutokana na kuwepo kwa shule ambazo kwa sababu mbalimbali zimepewa vibali vya kuendesha masomo kwa mfumo wa ‘double shift’,”alifafanua Mtahabwa.

Aliongeza: “Na kutokana na tatizo la usafiri kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule wanazosoma, Wizara inaelekeza shule zirejee kwenye ratiba zao za kawaida za vipindi nane kwa siku.”

Aidha, alisema iwapo uongozi wa shule utaona kuna sababu za msingi za kuongeza muda wa taaluma basi zitumike muda uliopangwa kwenye ratiba ya shule kwa ajili ya kutekeleza mtaala wa ziada au shughuli za nje ya darasa.

Juni 17, mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alitangaza mabadiliko ya ratiba za masomo katika shule za msingi na sekondari kwa kuongeza saa mbili kila siku kwa ajili ya kufidia muda uliopotea kutokana na mapumziko ya corona.

Imeandikwa na Fatma Mtutuma na Mary Mshami, UDOM

Habari Kubwa