Serikali yaiagiza TMDA kujengea uwezo watafiti

27Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yaiagiza TMDA kujengea uwezo watafiti

SERIKALI imeitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), kuhakikisha inawajengea uwezo watafiti wanaochipukia wakiwamo vijana waliopo vyuoni, ili kuongeza idadi ya watafiti na kuleta faida kwa taifa.

Aidha, imeitaka mamlaka hiyo, kufanya majaribio na utafiti wa uhakika wenye viwango vinavyostahili ili kutoa majibu yanayotarajia kwa dawa na vipimo vitakavyosaidia binadamu.
 
Maelekezo hayo yalitolewa jana, jijini Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuboresha mifumo ya kudhibiti majaribio ya dawa (ASCEND) katika utafiti mbalimbali unaofanyika nchini.
 
Alisema kwa sasa watahakikisha TMDA na vyombo vyake wanapunguza muda wa kuidhinisha dawa ili kutoa ruhusa ya kutumiwa.
 
“Kuna kipindi kuidhinishwa kwa dawa au vipimo ilikuwa inachelewa na kufika hata miezi miwili hadi mitatu, najua kulikuwa na changamoto ya kupata watu wa utafiti, lakini kupitia mradi huu itasaidia kujenga mfumo wa kuongeza spidi ya utafiti,” alisema Prof. Makubi.
 
Aidha, alisema TMDA na taasisi ziangalie suala la gharama la kuandikisha utafiti katika kupata matokeo ya utafiti wa dawa zinazoombwa hususani kwa wanafunzi wanaokuwa kwenye masomo vyuoni ambao wengi hawapati fedha nyingine.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, alisema mradi huo unahusisha taasisi saba za Tanzania Bara na Visiwani ikiwamo Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili (MUHAS).

Alisema baada ya kuandika andiko la mradi mamlaka imefanikiwa kupata fedha za kuteleza mradi huo kwa muda wa miaka miwili na nusu lengo likiwa ni kuimarisha mifumo ya udhibiti wa majaribio ya dawa, mifumo ya utafiti, namna ya kusoma na kupitisha maombi mbalimbali ya udhibiti wa majaribio ya dawa kabla ya kufanyika nchini.

Alisema pia mradi huo wa miaka miwili utasaidia kuweka mifumo mizuri ya kufuatilia madhara wanayopata watu watakaotumia dawa za majaribio.
 
Kadhalika alisema kupitia TMDA na MUHAS watatoa mafunzo kwa wataalamu mbalimbali waliopo ndani ya mamlaka ya udhibiti pamoja na wanaofanya majaribio ili kupata uelewa zaidi mpana katika masuala hayo.

Alisema jukumu lingine ni kuwa na fursa ya kupitia miongozo mbalimbali ambayo wataiboresha ili iwekwe sawa kati ya Tanzania Bara na Visiwani ili kutekeleza yale ambayo wamekusudia kuyafanya.

 
 

Habari Kubwa