Serikali yaja na utatuzi mazao ya mikunde kuuzwa stakabadhi ghalani

15Sep 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Serikali yaja na utatuzi mazao ya mikunde kuuzwa stakabadhi ghalani

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo, imeunda Timu ya watu Nane, ambayo itakusanya maoni na Mapendekezo kwa wakulima na wadau wa zao la mikunde, ili kutatua tatizo la uuzwaji wa mazao hayo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda, kushoto, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Shinyanga, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati.

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda, amebainisha hayo leo mkoani Shinyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuwa Serikali imeunda Timu ya kupitia mfumo wa mauzo ya mazao ya dengu, choroka, mbaazi, na ufuta, ili kuona hatua gani ya kuchukua ili mfumo wa stakabadhi ghalani ukitumika kusiwe na Buguza.

Alisema hivi karibuni kulitokea sintofahamu mkoani Shinyanga juu ya mauzo ya mazao hayo ya mikunde kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, ambapo waliwasiliana na uongozi wa mkoa huo, na kuamua kusitisha kwanza mfumo huo, ili kuangalia mambo gani wayaweke sawa kwanza.

“Hivi karibu mlisikiliza hotuba ya Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa wakati akihitimisha vikao vya bunge, alisema mwelekeo wetu ni kuelekea kwenye stakabadhi ghalani, lakini alielekeza Wizara ya kilimo kwamba tutengeneze mazingira mazuri, ili mfumo wa stakabadhi unapokuwa ukifanya kazi usiwe buguza kwa wakulima ambao wanauza mazao, na hii ni sehemu ya utekelezaji,”alisema Profesa Mkenda.

“Kitu cha kuzingatia kwenye timu hii, ni kutengeneza vigezo ambavyo vitafanya mazao haya ya mikunde kuingia kwenye mfumo wa Stakabadhi ghalani, kutumia utaratibu gani ambao utampatia pesa mkulima kwa wakati pale anapokuwa akiuza mazao yake kwenye mfumo huu,”aliongeza.

Aidha Waziri huyo wa Kilimo aliitaja Timu hiyo ya watu Nane, ambayo imepewa mwezi mmoja kukusanya maoni na mapendekezo hayo, kuwa inaongozwa na Mwenyekiti wake Dk. Hamisi MwinyiMvua kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam, na katibu wake Ernest Doriye kutoka Wizara ya Kilimo.

Pia, aliwataja wajumbe wengine wa Timu hiyo kuwa ni Dk, Anaciet Kashuliza, Barney Laseko, Dk. Ruhinduka Remedius, Dk. Wilhelm Ngasamiaku, Shaibu Chilavi na Samson Poneja, ambao watazungumza kwenye mikoa mitatu ya Shinyanga, Morogoro, pamoja na Lindi.

Habari Kubwa