Serikali yajipa wiki 2 malipo ya korosho

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Lindi
Nipashe
Serikali yajipa wiki 2 malipo ya korosho

SERIKALI imeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa kufikia mwisho wa mwezi huu, wakulima wote wa korosho watakuwa wamelipwa fedha zao baada ya uhakiki kukamilika kwa kiasi kikubwa.

Hakikisho hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alipotoa ufafanuzi katika mkutano uliowakutanisha wajumbe wa kamati hiyo, viongozi wa serikali, wataalamu na wakulima mkoani Lindi.

"Kumekuwa na urasimu mkubwa tangu kuanza kwa uhakiki, lakini sasa tumeamua kama serikali kabla ya mwisho wa mwezi huu wa tatu (mwezi huu), wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ili kuondoa adha wanazokumbana nazo," Hasunga alisema.

Waziri huyo alisema mchakato wa malipo unahitaji kupitia katika hatua nyingi ikiwamo uhakiki, lakini kila jambo lenye mwanzo ni lazima kuwa na ukomo.

Alibainisha kuwa mpaka sasa, tani 222,684 za korosho zimekusanywa na hadi kufikia Ijumaa iliyopita, Sh. bilioni 596.9 zilikuwa zimeshalipwa kwa wakulima kati ya Sh. bilioni 723 wanazodai.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Christine Ishengoma, alimwagiza waziri huyo kuhakikisha taarifa ya malipo ya wakulima wote wa korosho inafika bungeni Aprili 2, mwaka huu.

Hasunga pia alisema wizara imepitia hatua mbalimbali ya kumpata Mkurugenzi mpya wa Bodi ya Korosho ili kuendelea na majukumu ya bodi hiyo.

Alisema hatua mbalimbali pia zimeanza kuchukuliwa dhidi ya wafanyabiashara wote waliofanya hujuma kwa kuwauzia wakulima mbegu na mbolea feki.

Waziri huyo aliuagiza uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Tropiki (TPRI) kutuma wataalamu mkoani Lindi kuchukua sampuli za viuatilifu kwa wakulima na kuzipima ili kujua ukweli wa madai ya kuwapo kwa viuatilifu feki vilivyosambazwa kwa wakulima.

 

Habari Kubwa