Serikali yajivunia ongezeko la wanawake katika uongozi

22Feb 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yajivunia ongezeko la wanawake katika uongozi

SERIKALI imesema inajivunia ongezeko la wanawake kwenye nafasi za uongozi ikitolea mfano wa majaji wanawake ambao wameongezeka kutoka 24 mwaka 2015 hadi 40 mwaka jana.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Afya, Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Prudence Constantine, akizungumza na waadishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika jijini Dodoma tarehe 27 mwezi huu. Kushoto ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkuu wa Wizara hiyo, Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii, Erasto Ching’oro. PICHA: MIRAJI MSALA

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Wizara ya Afya, maendeleo ya Jasmii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prudence Constantine, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW).

Alikuwa akizungumzia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika Machi 8, kila mwaka duniani kote na kwa nchini mwaka huu zinafanyika kitaifa mkoani Simiyu.

Constantine alisema serikali imeendelea kutekeleza maazimio ya mkutano wa Beijing kwa kuweka mazingira wezeshi ya kukuza usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake.

Alisema serikali imeendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi kuondoa umaskini, kutoa elimu, mafunzo na ajira, kukuza ushiriki wao kwenye nafasi za uwakilishi na ngazi za maamuzi na kuwajengea uwezo katika sheria.

Pia alisema serikali imefanikisha kuanzishwa kwa mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na maendeleo ya wanawake wenye masharti nafuu ambao umesaidia kutoa mikopo nafuu na mafunzo ya stadi za biashara.

Alisema tangu mwaka 2015 serikali imeendelea kutoa Sh. bilioni 28.8 ambazo zimesaidia vikundi 13, 619 vya wanawake na kufanya idadi ya wanawake wajasiriamali walionufaika na fedha hizo kufikia 883,724.

Tanzania, alisema imefanya mabadiliko kwenye utoaji wa fedha za halmashauri kwaajili ya mikopo ya wanawake na marekebisho ya sheria ya fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya 2008 uchangiaji wa mikopo umekuwa wa kisheria.

Constantine alisema Tanzania jumla ya vikundi 19,874 vya wanawake wajasiriamali vimehamasishwa na kuanzishwa kwa kipindi cha mwaka 2017/18 na kwamba serikali imewezesha wanawake wajasiriamali kushiriki biashara na maonyesho ya kimataifa.

Pia alisema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kisheria kwa wanawake ili kuwawezesha kupata haki zao za msingi ikiwamo kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali na kutunga mpya kuwalinda.

Habari Kubwa