Serikali yakaza masharti kuikabili corona

26Jul 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yakaza masharti kuikabili corona

SERIKALI imetoa mwongozo mpya wa kupambana na corona, huku ikipiga marufuku mikusanyiko mikubwa ya kijamii, kama sherehe, kisiasa na kidini isiyo ya lazima hadi ugonjwa huo utakapodhibitiwa na taarifa kutolewa rasmi.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Abel Makubi, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Kutokana na mwenendo wa ugonjwa wa corona nchini, kamati ya wataalamu imeainisha maeneo mahususi yanayohitajika kutiliwa mkazo kupitia afua za kupunguza msongamano katika jamii, lengo ni kukata mnyororo wa maambukizi katika ngazi ya kaya na jamii,” alisema.

“Mwongozo huu utawawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii sambamba na kubadili tabia zao huku wakizingatia mbinu za kujikinga na ugonjwa, kwa kupata elimu ya kutosha na kujiwekea utaratibu wa kudhibiti ugonjwa kutokusambaa kwenye jamii.”

Alisema pale ambapo patahitajika kufanyika shughuli za mikusanyiko, kutatakiwa kuombwa kibali maalum.

“Maeneo yanayoleta mikusanyiko ni yale ya huduma za kijamii, kibiashara, kiuchumi, kiofisi, ambayo ni mojawapo ya vyanzo vya kusambaa kwa maambukizi katika jamii. Mwongozo huu unalenga kudhibiti ugonjwa huu bila kuathiri shughuli za kiuchumi na maisha ya kawaida ya kijamii ya wananchi.”

Pia, alitaka wasafiri wawezeshwe kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kabla ya kuingia kwenye vyombo hivyo vya usafiri.

Mwongozo huo unawataka viongozi wa mtaa husika kuhakikisha kila kituo kunawekwa vyombo vya kuhifadhia maji na sabuni vya kutosha.

Kwenye vituo vya mabasi, unaelekeza uongozi wa vituo hivyo, kusimamia uwapo wa vifaa vya kunawia kwa maji tiririka na kuhakikisha abiria wote wananawa mikono.

Unawaelekeza pia wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha wanaweka vipukusi vya kutakasa mikono katika vyombo vya usafiri na kusimamia uvaaji barakoa.

BARAKOA LAZIMA

“Abiria wote waendelee kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutosongamana ndani ya vituo vya mabasi kupitia walinzi getini, wahudumu wa mabasi na askari wa usalama wa barabarani.

“Stendi zihakikishe zinatoa ujumbe wa kuelimisha jamii ya wasafiri mara kwa mara kupitia vipaza sauti, na wanapokuwa safarini, madereva na wahudumu wa vyombo vya usafiri wahakikishe ujumbe wa kuelimisha unatolewa kwenye chombo mara kwa mara.”

MARUFUKU ABIRIA KUSIMAMA

“Vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe magari ya usafiri wa umma wanapakia abiria kulingana na idadi ya viti pasipo kusimama, kwa magari maalumu yenye nafasi kubwa kama mwendokasi, inapolazimika kusimama basi kila abiria avae barakoa na kuachiana angalau umbali wa nusu mita,” alisema Profesa Makubi.

UPIMAJI

“Upimaji wa dalili za ugonjwa wa corona na taratibu getini wakati wa kuingia/kutoka ndani ya mabasi. Kupima joto mwili kwa kutumia ‘thermoscanners’ ufanyike getini na kwenye mabasi.”

NYUMBA ZA IBADA

Mwongozo huo mpya unaelekeza nyumba za ibada kukaguliwa mara kwa mara, kuweka vifaa vya kunawia na maji tiririka, waumini kuvaa barakoa, na kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja na mwingine na kuwapo na utaratibu wa utakasaji wa viti, meza na maeneo wanayokaa kabla na baada ya ibada.
 
“Wazee, watoto na wale wote wenye matatizo ya kiafya yanayotambulika ikiwamo kisukari, shinikizo la damu, saratani, wanashauriwa kujiepusha na ibada zenye mikusanyiko ya watu wengi na wachukue tahadhari zote muda wote,” alisisitiza.

“Ibada ziwe za muda mfupi usiozidi saa mbili. Huduma zinazohusisha kugusana ziepukwe. Kuwapo na ujumbe wa mara kwa mara kwa ajili ya kuwakumbusha waumini kuhusu namna ya kujikinga.”

KUMBI ZA STAREHE

“Maeneo ya baa, migahawa, hoteli, kumbi za starehe, mikutano, harusi na sherehe mbalimbali kimsingi baadhi ya shughuli za kundi hili zinafaa kuangaliwa iwapo ni muhimu, za lazima au zisubiri hali itengemae. Iwapo ni muhimu na lazima kuwe na kipima joto kwa wote wanaoingia kupata huduma kwenye eneo husika.”

“Sherehe zote za harusi kufanyika nje ya kumbi au kama zinafanyika ukumbini, ziwe za muda fupi, wageni waalikwa wawe wachache kuruhusu ukaaji wa mita moja au zaidi.”

VITUO VYA AFYA

Mwongozo huo unaelekeza kwamba wagonjwa wa nje wasio na dharura waonwe kwa kupangiwa tarehe maalumu ili kuzuia mrundikano kwa wagonjwa kwa wakati mmoja na kwamba wagonjwa wenye magonjwa sugu wapewe dawa za angalau miezi miwili.

VITUO VYA POLISI NA MAGEREZA

Mwongozo huo unaelekeza vituo hivyo kutoa kipaumbele cha dhamana kwa mahabusu wenye makosa yanayodhaminika kisheria ili kupunguza msongamano na kuruhusu ndugu mmoja tu kumtembelea mfungwa katika siku iliyotengwa na kuwataka wasikilizaji wa kesi kuvaa barakoa na kukaa kwa umbali.

MASOKONI

Mwongozo kwenye masoko unatelekeza halmashauri ziandae timu za kukagua maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na kutumia viwanja vya mipira wa miguu au maeneo yoyote yaliyo wazi kwa ajili ya huduma za masoko au kushushia bidhaa.