Serikali yalinda wazalishaji wa vifaa vya umeme

12Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yalinda wazalishaji wa vifaa vya umeme

WAZIRI wa Nishati, Medard Kalemani, ametangaza serikali kuzuia uingizaji holela wa viunganishi vya umeme kutoka nje ya nchi ili kuchochea uwekezaji katika kuzalisha vifaa vya umeme nchini.

Aidha, hatua hiyo ni ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda cha Polymeric Insulator cha jijini Dar es Salaam ambacho kinatengeneza vifaa vya kuunganisha mifumo ya umeme, Waziri Kalemani alisema kuwa mbali ya zuio hilo, serikali itawahakikishia wawekezaji hao soko la ndani la vifaa vyao vya umeme.

“Tangu mwaka 2017 tumewema mazuio kadhaa katika kuhakikisha vifaa vya umeme vinazalishwa hapa nchini ili kuunga mkono juhudi za serikali za ujenzi wa viwanda. Pamoja na mazuio hayo, leo (jana) natangaza kuzuia uingizwaji holela wa vifaa vya kuunganisha mifumo ya umeme (insulators) kwa lengo la kuchochea uwekezaji katika eneo hilo,’’ alisema.

Alikisifu kiwanda hicho kwa kuzalisha vifaa hivyo na kusema lazima kuungwe mkono kwani hatua hiyo inaongeza upatikanaji wa ajira kwa vijana na kukuza pato la Taifa.

Aidha, ametaka Shirika la Umeme (TANESCO), Wakala wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) kushirikiana na Shirika la Viwango (TBS) kuhakikisha viwanda vinazalisha vifaa vyenye ubora na uwezo wa kushindana katika soko huria na kuwalinda watumiaji.

“Pamoja na kuhimiza uwekezaji katika viwanda, vyombo husika kama Tanesco, TBS na REA lazima vihakikishe bidhaa bora zinazalishwa ili kuwalinda watumiaji wa bidhaa zinazozalishwa ndani,” alisema.

Mshauri Maalum wa viwanda cha Polymeric and Inhemeter, Dk. Adelhelm Meru, alisisitiza umuhimu wa taasisi nchini kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani kwani kwa kufanya hivyo zitakuwa zinachangia kudumisha ajira na kusaidia ukuaji wa uchumi.

“Hivi karibuni Tanzania iliingia uchumi wa kati, hivyo ni muhimu kuhimiza uzalishaji viwandani ili kuendelea kujenga uchumi imara na kukuza ajira,’’ alisema Dk. Meru.

Dk. Meru aliyataka mashirika ya umma kuacha kuagiza vifaa vya umeme kutoka nje. Na kushauri kampuni ya nje kuwekeza nchini kwa kuwa mazingira ya uwekezaji yamerahisishwa sana.

“Serikali imefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha panakuwapo na mazingira rafiki ya uwekezaji, hivyo nashauri mashirika ya umma yahimize wawekezaji kuja kuwekeza nchini badala ya kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,’’ amesema katibu mkuu mstaafu wa wizara mbali mbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Abraham Rajakili, aliishukuru serikali kwa kuwaunga mkono na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, hatua hiyo imewarahisishia kwa kiwango kikubwa kufikia malengo yao.

Habari Kubwa