Serikali yamjibu mbunge mvuto wafanyakazi ATCL

09Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Serikali yamjibu mbunge mvuto wafanyakazi ATCL

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, amesema serikali haitumii kigezo cha mvuto katika kuajiri watumishi wa Shirika la Ndege (ATCL).

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, picha mtandao

Nditiye alitoa kauli hiyo jana bungeni, baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Husna Mwilima, kusema juzi kuwa kuna haja shirika kuajiri wahudumu wenye mvuto.

Kabla ya kujibu maswali yaliyoelekezwa wizarani kwake bungeni jana, Nditiye alisema serikali na shirika hilo wameainisha sifa mbalimbali za kuajiri, ikiwa ni pamoja na kigezo cha kuwa Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18.

Alivitaja vigezo vingine kuwa ni kuwa na ufahamu wa lugha za Kingereza na Kiswahili kwa ufasaha na kuwa na cheti cha kuongoza ndege ama cha kufanya kazi ndani ya ndege.

Nditiye alisema sifa nyingine za ziada ni kuwa na ufahamu na mambo mbalimbali ya kitaifa, kidunia na utalii. Alisema pia anatakiwa kuwa na hekima, heshima, maadili na huchunguza kama anafaa kuajiriwa.

Mbunge wa Igalula, Mussa Ntimizi (CCM), alikuwa miongoni mwa wabunge waliouliza maswali yanayoihusu wizara hiyo, akitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali ili wananchi wa jimbo lake wapate huduma ya mawasiliano ya simu.

Akijibu swali hilo, Nditiye alisema serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano nchi nzima.

Alisema Julai mwaka huu, mfuko ulitangaza zabuni ya awamu ya nne kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata 521 zenye vijiji 1,222.

Alisema Kata ya Tura iliyoko katika jimbo la mbunge huyo, ilijumuishwa kwenye zabuni ikiwa na vijiji vya Karangasi, Mmunyu na Mwamlela na kwamba imeshafunguliwa na baada ya tathmini, mzabuni atapatikana katika maeneo hayo.

Alisema utekelezaji wa mradi huo utaanza baada ya mkataba kutiwa saini mwezi ujao.

Habari Kubwa