Serikali yamwaga ajira 610 madaktari

25Mar 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Serikali yamwaga ajira 610 madaktari

SERIKALI imetangaza ajira za madaktari 610 ili kujaza nafasi kwenye hospitali za Halmashauri na vituo vya afya nchini.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Nyamhanga, picha mtandao

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa Februari mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Madaktari Duniani, ya kutoa ajira mpya kwa madaktari 1,000 nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Nyamhanga, madaktari watakaoajiriwa ni wa binadamu na meno waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya Elimu ya Juu vinavyotambulika na serikali.

“Tamisemi imepata kibali cha kuajiri kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa madaktari na wataanza leo(jana) kuwasilisha maombi yao na waombaji wawe tayari kufanya kazi Halmashauri yoyote watakayopangiwa,” alisema.

Aliongeza: “Maombi yote yatumwe kwa njia ya mtandao (online) kupitia mfumo wa kielektroniki unaopatikana kupitia anuani ya ajira.tamisemi.go.tz. na maombi yoyote yatakayowasilishwa kwa njia ya posta au kuletwa moja kwa moja ofisini hayatafanyiwa kazi.”

Alisema mwisho wa kupokea maombi ni Aprili, 10 mwaka 2020 saa 9:30 alasiri.

Akizungumza katika mkutano wa madaktari pamoja na watumishi wa sekta ya afya uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema anafahamu kuna madaktari takribani 2,700 hawajaajiriwa.

“Nitalifanyia kazi. Nafikiri tunaweza tukaanza polepole hata tukachukua 1,000 eti Waziri wa Utumishi (George Mkuchika) hatuwezi kuajiri hata 1000, hela si zipo kidogo? Basi tuajiri 1,000 madaktari, tuanze na 1,000 mambo yakiwa mazuri tena tunaajiri wengine kwa sababu tunahitaji madaktari mpaka vijijini,” alisema.

Habari Kubwa