Serikali yaombwa kujenga ofisi ya Afisa Maendeleo ya Jamii Mwanza

25Nov 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
Serikali yaombwa kujenga ofisi ya Afisa Maendeleo ya Jamii Mwanza

WATAALAMU wa Ustawi wa Jamii wameiomba serikali kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga ofisi ya afisa maendeleo ya jamii ili aweze kutoa nafasi kwa watu kueleza matatizo katika hali ya faragha na pia kuwepo sehemu ya kutunzia nyaraka za wateja.

Hayo yamezungumzwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii Dk Mariam Mahuu, wakati wa Kongamano la kitaifa la ustawi wa jamii na mkutano mkuu wa chama cha wataalamu wa ustawi wa jamii lililokutanisha jumla ya washiriki 300 jana Jijini Mwanza kwa lengo la kujadili kanuni mbalimbali za uendeshaji wa majukumu na namna ya kukabiliana na changamoto za kazi.

"Hakuna maeneo, Afisa hana ofisi yake peke yake, unakuta wamekaa kama timu na mtu anapokwenda pale sio rahisi kutoa ama kueleza matatizo yake kwa afisa kwa sababu pale unapoingia unaenda kwa daktari wa jamii ambaye anataka achimbe ajue chanzo cha tatizo ni nini, nani amehusika sasa unapoingia wewe kama ni mteja yale mazingira ukikuta ni maafisa ustawi wapo kama kumi utaweza kuongea”, amehoji Dk Mahuu.

Dk Mahuu amesema uwepo wa Ofisi utawarahisishia maafisa ustawi kazi ya kuwahudumia wananchi katika hali ya usiri hivyo wanapojenga majengo ya Ofisi mpya wahakikishe wanatenga kabisa eneo kwa ajili ya Ofisi ya afisa ustawi wa jamii.

Kwa upande wake mshiriki Faithmary Lukindo Afisa Ustawi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema pamoja na upungufu wa ofisi bado idadi ya maafisa ustawi walioajiriwa haitoshi hivyo serikali iongeze juhudi katika kuwaajiri ili kuendelea kuhudumia jamii na kutatua changamoto zao.

"Sisi Kama maafisa ustawi wa jamii kwa sababu ya umuhimu wa kazi zetu katika jamii tunaomba serikali iajiri maafisa ustawi wa jamii wengi zaidi ili tuendelee kuhudumia jamii pamoja na kutatua changamoto zao" amesema Faithmary.

Habari Kubwa