Serikali yaonya kampuni za bima afya udanganyifu

18Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Serikali yaonya kampuni za bima afya udanganyifu

SERIKALI imewaonya watu wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu katika sekta ya bima ya afya nchini, vinavyofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile (kulia), akipokea cheti cha shukurani kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampuni Binafsi za Bima ya Afya, Violet Mordichai, katika mkutano wa wadau wa bima ya afya nchini, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: MPICHAPICHA WETU

Onyo hilo lilitolewa Dar es Salaam, jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, ambaye alisema serikali inatambua kuwa udanganyifu huo hufanywa na baadhi ya watoa huduma za afya na watu wanaotibiwa kwa mfumo huo.

 

Ndugulile alikuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Kampuni za Bima ya Afya Tanzania (ATI).

 

Aliongeza kuwa wakati mwingine vitendo hivyo hufanywa kwa ushirikiano kati ya wafanyakazi wasio waaminifu pamoja na wateja.

 

Dk. Ndugulile alitoa onyo kwa wanaojihusisha na udanganyifu kwa lengo la kuhujumu huduma za bima ya afya, kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai na adhabu yake ni kifungo jela pamoja na faini.

 

“Serikali ya awamu ya tano, chini ya uongozi wa Dk. John Magufuli, inapinga kwa vitendo rushwa na udanganyifu na yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo huchukuliwa hatua kali za kisheria. Serikali hii imeelekeza nguvu zake katika kujenga mfumo na taifa lenye uadilifu,” aliongeza.

Alitoa wito kwa kila mwananchi kuwa mlinzi wa sekta ya afya kwa kutoa taarifa sahihi za vitendo vya udanganyifu kwa vyombo husika, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

 

Aidha, alisema serikali inathamini mchango wa kampuni za bima ya afya nchini na kwamba inaendelea kuhakikisha kuwa kuna mazingira rafiki ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma, ili kuhuisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa bei nafuu kwa kila Mtanzania.

 

Aliongeza kuwa ingawa kiwango cha watu wanaojiunga na huduma ya afya nchini kinaongezeka, hadi sasa ni asilimia 32 tu ya Watanzania wote ndio walipo katika mfumo wa bima ya afya na wengi wao ni wanaoishi mijini; wakati malengo ya afya kwa wote ni kufikia asilimia 70 ya Watanzania kufikia 2020. Hivyo, alisema kiwango hicho bado hakiridhishi.

 

Alisema ili kuhakikisha kuwa lengo hilo linatimia, pamoja na kutoa elimu na uhamasishaji, serikali iko kwenye mchakato wa kuandaa muswada wa sheria itakayomtaka kila Mtanzania kuwa na bima ya afya na kwamba anaamini mwaka kesho inaweza kupitishwa na Bunge.

 

“Nitumie fursa hii pia kuwahamasisha wananchi wote kuwekeza katika bima ya afya kwa kujiunga na mifuko ya bima ya afya, kwa sababu hakuna jambo muhimu kwa ustawi wa jamii kama kuwa na uhakika wa kupata huduma stahiki za matibabu wakati wowote,” alisema.

 

Awali, Mwenyekiti wa ATI, Suleiman Khamis, aliipongeza serikali kwa juhudi za kuboresha huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na huduma bora ya bima afya.

 

Alisema majadiliano katika mkutano huo uliowahusisha wadau wa sekta binafsi na umma umehuisha utatuzi wa changamoto ya udanganyifu utakaoweka mfumo bora wa utoaji taarifa; pamoja na kuwa na viwango sawia vya gharama ya huduma kwa bima afya.

 

Elia Kajiba, aliyemwakilisha Kamishna wa Shughuli za Bima (TIRA), Dk. Baghayo Saqware, aliwataka wadau wa sekta ya bima nchini kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Bima ya Mwaka 2009.

 

Alisema kuwa mamkala hiyo inaendelea kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya usimamizi wa sheria na inachukua hatua kali kwa wanaoenda kinyume na sheria, kwa kuwa ukosefu wa uadilifu ni tishio la ustawi wa taifa.

Habari Kubwa