Serikali yaonya matumizi fedha mikopo kwa wanafunzi vyuo vikuu

16Oct 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Serikali yaonya matumizi fedha mikopo kwa wanafunzi vyuo vikuu

SERIKALI imetoa maagizo mazito kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), ikitaka kuhakikisha fedha zlizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, zinawafikia walengwa kwa wak

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo, PICHA MTANDAO

Katika mwaka wa fedha wa 2020/21, serikali imetenga Sh. bilioni 464 kwa mikopo ya wanafunzi wanaojiunga katika vyuo vikuu na wale wanaoendelea na kozi mbalimbali.

Pia serikali imewataka maofisa mikopo kuhakikisha kuwa wanaratibu vizuri utoaji wa mikopo na ufuatiliaji wa marejesho kwa wanufaika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo, aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akifungua kikao kazi cha menejimenti ya HESLB na maofisa wanaosimamia mikopo vyuoni.

Dk. Akwilapo alisema fedha zilizotengwa kwa msimu huu, zimelenga kuwanufaisha wanafunzi 145,000 wanaosoma katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.

Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kimekuwa kikiongezeka kila mwaka, ili kutoa fursa kwa vijana wengi wa Kitanzania kupata mikopo ya elimu ya juu, ili watimize ndoto zao.

“Kiasi hichi kimepanda ukilinganisha na kile cha mwaka fedha 2014/15, ambacho ilikuwa Sh. bilioni 347. Hali hii inaonyesha ni namna gani serikali ambavyo imedhamiria kuwezesha vijana wa kitanzania kupata elimu bila kuwa na usumbufu wowote,” alisema Dk. Akwilapo.

Pia aliwataka maofisa mikopo vyuoni kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuhakikisha wanafanya katika mazingira ya utulivu, bila kuwapo malalamiko yoyote.

“Katika miaka iliyopita pamekuwapo na utulivu katika utoaji wa mikopo, hivyo nawataka maofisa mikopo wote pamoja na vyuo kuhakikisha zoezi hili lifanyika kwa utulivu na wanafunzi wote, wanashughulikiwa nisingependa kusikia malalamiko yoyote,” alisema.

Vievile, aliagiza vyuo vikuu nchini vinapopokea fedha hizo, visikae nazo katika akaunti zao bali wawapatie wanafunzi waliokidhi vigezo, bila kuwawekea vikwazo.

Dk. Akwilapo pia alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano, imetumia Sh. trilioni 2.25 kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi mbalimbali wa elimu ya juu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdulrazaq Badru, alisema watahakikisha kuwa kabla ya vyuo vikuu, kufunguliwa mwezi ujao, fedha hizo zitakuwa zimewafikiwa wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo.

Badru alisema utaratibu wa madawati ya maofisa mikopo vyuoni ulianzishwa na serikali rasmi mwaka 2011, ili kusimamia na kuwezesha mikopo na hivi sasa pia yanaratibu urejeshaji wa mikopo.

Alifafanua kuwa katika kikao kazi hicho, kinachoshirikisha maofisa mikopo vyuoni zaidi ya 120, pia mada mbalimbali zitajadiliwa, ikiwamo ulipaji mikopo kidigitali na ufafanuzi wa tozo mbalimbali za mikopo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HESLB, Prof. William Anangisye, aliwataka maofisa mikopo kutumia lugha zenye staha kwa wanafunzi wakati wanapo wahudumia.

Alisema si jambo la busara kusikia kuwa kunakuwepo na malalamiko kwa wanafunzi kuwa maofisa mikopo wanatumia lugha mbaya kwao wakati wa kuwahudumia.

“Wanafunzi wamekuwa wakienda katika vyombo vya habari kulalamika kutokana na nyinyi maofisa mikopo kutoa lugha chafu kwao lazima mfanye kazi kwa kuheshimiana bila kujali nafasi zenu,” alisema Prof. Anangisye.

Habari Kubwa