Serikali yaonya viongozi wa dini matamko binafsi

01Aug 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yaonya viongozi wa dini matamko binafsi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wa dini nchini kujiepusha na matamko binafsi yenye lengo la kusababisha vurugu kwenye dini na taifa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa tatu kushoto), akishiriki katika Swala ya Eid El Hajj, iliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, jana. Wa pili kushoto ni Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Zubeir Bin Ally na wa nne kushoto ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum. PICHA: JUMANNE JUMA

Vilevile, amesema serikali imeunda tume iliyohusisa wakuu wa mikoa kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha shule za kiislam nchini kuungua moto.

Majaliwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika Baraza la Eid El-adh’haa liliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Alisema matamko ya watu binafsi yenye dhana ya kubeba maoni binafsi, kuyachanganya na msimamo wa jumuiya au dini ni jambo linaloweza kusababisha machafuko nchini.

“Wewe peke yako umewaza, kwa utashi wako, ukaenda mbele ukaaminisha kuwa hili tamko ni la wote. Muhimu sana tuwe na tahadhari hiyo,” alionya Majaliwa.

Alisisitiza viongozi wa dini kuendeleza mshikamano na taasisi za dini na nyingine za kiraia, ili kuendelea kujenga umoja wa taifa.

“Mheshimiwa Mufti kama kiongozi wetu mkuu, unafanya kazi nzuri sana, umetuunganisha, umetunasihi, usisahau pia kutukemea panapotakiwa kuturekebisha, turekebishe,” alisema.

Majaliwa alisema wapo viogozi ambao wanaaminika na jamii na wanapotoa matamko binafsi yanayotaka kuaminisha ni msimamo wa dini ya kiislam na yanaleta taharuki.

Majaliwa alionya kuwa serikali haitawafumbia macho viongozi kama hao ambao wanazungumza mambo ambayo hayapo na yenye mlengo wa kuharibu amani ya nchi.

Kuhusu matukio hayo ya moto, Majaliwa alisema ameshamwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge, kuunda tume ya kufanya uchunguzi katika shule zote ambazo ziliungua ili kufahamu chanzo chake.

“Tume inakamilisha ripoti ya matukio haya na tutatoa taarifa na serikali haitawafumbia macho watakaobainika walihusika katika matukio hayo ama kwa njama. Na kama ni makosa yalifanyika, tutawaeleza,” alisema Majaliwa.

Alisema shule za dini zina maslahi na taifa, hivyo hakuna sababu ya kulifumbia macho suala hilo.

Awali, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi, alimwomba Majaliwa kusimamia uchunguzi uliofanyika kuhusu kuungua mfululizo kwa shule za dini ya kiislam nchini.

Alisema wanapata shaka kutokana na mazingira ya shule hizo kuungua kwa mfululizo na kwamba wameshindwa kulifumbia macho suala hilo.

“Shule zimeungua saba, hatujui chanzo chake, tumeshtushwa na idadi na mfululizo. Tunapata wasiwasi kwa nini zimeungua kwa wakati mmoja na kwa nini shule hizo tu. Tunaomba tujue tume inayochunguza itupe matokeo ya sababu za kuungua kwa shule hizo,” alisema Sheikh Zuber.

UCHAGUZI HURU

Katika baraza hilo, Majaliwa pia alisema Rais John Magufuli ameshawahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, utakuwa wa huru na haki na hivyo Watanzania wanatakiwa kuamini hivyo badala ya kuendelea kujengeana hofu.

“Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa huru na wa haki. Kwa hiyo, twende na hilo, tusianze kujengeana shaka, uchaguzi kuwa huru na haki inawezekana na ninawaambia inawezekana,” alisema Majaliwa.

Alisema viongozi wa dini wana wajibu wa kuendelea kuliombea taifa ili uchaguzi huo umalizike salama na wajiepushe na lugha za uchochezi.

Aliwasihi wanasiasa kuzungumza hoja za watakachofanya endapo watachaguliwa badala ya kuzungumza matusi na maneno ya kashfa.

Majaliwa alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, watu mbalimbali wamejitokeza kuwania nafasi za uongozi bila kuangalia itikadi za kidini.

HAKUNA CORONA

Majaliwa pia aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuliombea taifa wakati wa ugonjwa wa corona, akiamini maombi yamewezesha kutoweka kwake na kwamba hadi jana hakukuwa na mgonjwa katika hospitali zote nchini.

Alisema Rais Magufuli ndiye aliwatoa hofu Watanzania na viongozi wa dini ambao walishirikiana naye kuondoa hofu iliyokuwa imelikumba taifa.

“Bado kuna mataifa yanaendelea kutikisika, sisi tumepata mgonjwa wa kwanza Machi mwaka huu, tulitikisika kweli kweli na tukaingia kwenye tafrani kwa sababu tu wale wakubwa (nchi zilizoendelea), waliingia kwenye tafrani,” alisema Majaliwa.

Alisema Watanzania walijenga hofu nzito kwa sababu ya kujilinganisha na mataifa mengine kiuchumi ambayo yameidizi Tanzania, lakini walizidiwa na ugonjwa huo.

“Viongozi wa dini hatusiti kushukuru na Mwenyezi Mungu alimwongoza Rais Magufuli, kumpa maono na kumwambia atoke hadharani, sema hili, wape faraja Watanzania.

"Alipokuja kutusihi tuwe watulivu, tupunguze hofu na kwamba ugonjwa huu ni wa kawaida. Aliposema tu ni wa kawaida wapo walioelewa na wapo ambao hawakuelewa na nyie viongozi wa dini mlitoka mkamsaidia Rais kuhimiza watu kuondoa hofu,” alisifu.

Aliwataka Watanzania kupuuza habari za uzushi kuwa Tanzania kuna corona kwa sababu zina lengo la uchonganishi na mataifa mengine.

Majaliwa pia alisema kwa maombi ya viongozi wa dini, Mungu aliliepusha taifa na majanga ya nzige ambao kama wangeingia nchini, wangesababisha madhara makubwa.

Habari Kubwa