Serikali yapata dawa matatizo sugu ushirika

19Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Serikali yapata dawa matatizo sugu ushirika

SERIKALI imesema kumekuwa na mitazamo tofauti miongoni mwa wadau kuhusu sababu ya kuwapo kwa matatizo sugu ya ushirika na namna ya kushughulikia.

Wadau wengi wa ushirika nchini wamekuwa na mtazamo kwamba matatizo sugu ya ushirika nchini yanatokana na sababu mbalimbali na miongoni mwake ni upungufu wa sheria inayosimamia sekta ya ushirika nchini, Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013.

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, alisema jana mkoani Dar ers Salaam kuwa kwa sasa serikali imekuja na mwarobaini wa kutatua matatizo hayo.

Prof. Mkenda alikuwa anafungua kikao cha wadau wazoefu wa ushirika kujadili mapendekezo na marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013.

Waziri Mkenda alisema kufuatia mtazamo wa wadau na dhamira ya kutatua matatizo sugu ya ushirika yanayotokana na upungufu wa sheria, mwaka 2019 serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilielekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuanza mchakato wa kufanya mapitio ya Sheria ya Vyama Vya Ushirika.

Katika mkutano huo, Waziri Mkenda alimpongeza Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dk. Benson Ndiege, kwa kufanikiwa kuwaalika wadau wote wazoefu katika kikao hicho kwa ajili ya kutoa maoni.

Vilevile, Waziri Mkenda ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na Wizara ya Kilimo kuhakikisha maoni yatakayotolewa na wadau katika kikao hicho yanazingatiwa katika mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Ushirika unaoendelea.