Serikali yapata dawa ya kunufaika na bahari kuu

21May 2020
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Serikali yapata dawa ya kunufaika na bahari kuu

SERIKALI imekuja na mkakati wa kudumu wa kuiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zilizopo katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu, kwa kufuta Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 1998 na kutunga sheria mpya.

Akiwasilisha bungeni jijini hapa jana Muswada wa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu wa Mwaka 2020, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema sheria hiyo ni mwendelezo wa jitihada za serikali kuweka mazingira bora ya uwekezaji na usimamizi katika uvuvi wa Bahari Kuu.

Waziri Mpina alisema mbali na kutungwa kwa sheria hiyo mpya, Serikali ya Jamhuri wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zinatekeleza mikakati mbalimbali ikiwamo kufufua mashirika ya uvuvi yaani TAFICO na ZAFICO, akibainisha kuwa ununuzi wa meli kwa ajili ya uvuvi wa Bahari Kuu uko katika hatua mbalimbali huku ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ukiwa katika hatua za mwisho za upembuzi yakinifu.

Alitaja sababu za kutungwa kwa sheria hiyo mpya kuwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vilivyoonekana katika sheria ya zamani ikiwamo kutokuzingatia masuala muhimu ya kusimamia meli za uvuvi zinazopeperusha bendera ya Tanzania nje ya mipaka ya bahari ya Tanzania.

Pia, sheria hiyo ya zamani kutozingatia suala la uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi (conservation and management measures), udhibiti wa uvuvi haramu (Illegal Unreported and unregulated fishing - IUU), udhibiti wa bandari (port state measures) pamoja na uwezo wa mawaziri wenye dhamana kuingia mikataba ya uvuvi (bilateral fishing agreements).

Kutowapo masharti ya ukusanyaji na ubadilishanaji wa taarifa za uvuvi na mavuno ya samaki na uhifadhi wa mazingira ya EEZ na vivutio (incentives) kwa wavuvi na wawekezaji wa Kitanzania.

Waziri Mpina alisema matarajio ya serikali kwa kutungwa kwa sheria hiyo mpya ni pamoja na kuchochea uwekezaji katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na rasilimali za uvuvi wa Bahari Kuu.

Pia, sheria hiyo mpya itawezesha kuimarika kwa uhusiano wa kikanda na kimataifa kutokana na kupungua kwa matokeo ya uvuvi haramu na kuimarika udhibiti na ufuatiliaji wa meli za uvuvi zinazopeperusha bendera ya Tanzania zinapovua nje ya mipaka ya nchi katika Bahari Kuu (High Seas) na EEZ za nchi nyingine.

“Matokeo mengine ni kuimarika kwa mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za uvuvi na mavuno ya samaki utakaounganisha taarifa za maji ya ndani, maji ya kitaifa na eneo la Ukanda wa Uchumi wa Bahari na kupelekea kuongezeka kwa uwekezaji kwenye sekta ya uvuvi," alifafanua.

Waziri Mpina pia alisema sheria mpya itawezesha kuimarika kwa viwango vya utekelezaji wa taratibu na miongozo ya kikanda na kupungua kwa makosa yatokanayo na ukiukwaji wa sheria nchini.

Alisema madhara yaliyojitokeza kwenye sheria iliyofutwa ya mwaka 1998 ni pamoja na kukosekana kwa utaratibu wa usimamizi wa meli za uvuvi zinazopeperusha bendera ya Tanzania, hali iliyosababisha kukosekana ufuatiliaji wa karibu na kusababisha meli zinazovua nje ya Tanzania kuhusishwa na uvuvi haramu ikiwamo Meli ya Haleluya inayopeperusha bendera ya Tanzania nchini Colombia na kuhusishwa na uvuvi wa papa kinyume cha sheria.

"Katika mwaka 2020/2021, serikali itanunua meli tatu za uvuvi na kuanza uvuvi wa Bahari Kuu na maeneo mengine; kujenga na kuendesha viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi; kuendelea na ukarabati wa majengo na miundombinu ya Tafico itakayojumuisha gati la kuegeshea meli za uvuvi, kusimika mitambo ya barafu, maghala ya baridi pamoja na kuiwezesha Tafico kuanza miradi ya ukuzaji viumbe maji.

"Pia, katika juhudi za kuwezesha ujenzi wa bandari ya uvuvi, mazungumzo yanaendelea baina ya Serikali ya Tanzania na Korea ya Kusini kwa ajili ya kupata ufadhili wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika eneo litakalopendekezwa katika mwaka 2020/2021. Serikali itakamilisha upembuzi wa kina na kuanza ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika eneo litakalochaguliwa.

"Uwapo wa Bandari ya Uvuvi utawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga, kushusha mazao ya uvuvi na kupata huduma mbalimbali zikiwamo mafuta na chakula," alisema.

Wakati huo, Bunge limetaka kuwapo na udhibiti wa uvuvi wa papa katika bahari kuu, kutokana na watu kutumia mapezi yake kwa ajili ya supu na tiba asili.

Pia, limependekeza kuwa mtu yeyote atakayekutwa na mapezi ya papa bila ya kuwa na mwili atakuwa ametenda kosa kisheria.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilitoa mapendekezo hayo jana bungeni, ilipowasilisha maoni na ushauri kuhusu Muswada wa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu wa Mwaka 2020.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Ritta Kabati, akisoma maoni hayo, alisema kuna haja kuwekwa kwa masharti ya udhibiti wa samaki aina ya papa katika sheria hiyo.

Kabati alisema muswada huo hauna masharti kuhusiana na samaki hao na kwamba wamekuwa wakivuliwa sana duniani na kukatwa mapezi kwa ajili ya supu na tiba za asili hususani kwa soko la China na sehemu yote ya mwili iliobaki hutupwa baharini.

“Kwa mujibu wa kanuni za uvuvi wa bahari kuu zinazotumika hivi sasa, zinabainisha kuwa mtu yeyote atakayekutwa na mapezi ya papa bila kuwa na mwili atakuwa ametenda kosa kisheria,” alisema Kabati na kuongeza:

“Kanuni hizo zinafafanua zaidi kuwa iwapo mtuhumiwa atakutwa na hatia adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi bilioni moja au kifungo cha miaka 10 ishirini au adhabu zote kwa pamoja."

Alisema utaratibu wa mtu anayekutwa na mapezi ya samaki aina ya papa kuwa ni kosa la jinai unatumika katika nchi nyingi duniani kwa sababu mbalimbali.

Alisema miongoni mwa sababu hizo ni utunzaji wa mazingira ya baharini, kulinda baadhi ya aina za papa ambao wanatajwa kuwa hatarini kutoweka.

Alisema watetezi wa haki za viumbe hao wanaeleza kuwa ni ukatili kumkata papa mapezi na kumtupa baharini akiwa hana uwezo wa kuogelea.

“Kwa misingi hiyo, kamati inapendekeza kuwa, ni vyema masharti ya kuwalinda samaki aina ya papa yakazingatiwa katika muswada huu,” alisema.

Habari Kubwa