Serikali yapokea bil. 17/- gawio CRDB

11Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Serikali yapokea bil. 17/- gawio CRDB

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, jana alipokea gawio la Sh. bilioni 17 linalotokana na uwekezaji wa serikali katika ya Benki ya CRDB.

Makabidhiano hayo ya hundi kifani ya gawio hilo yalifanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha Dodoma na kuhudhuriwa na mawaziri na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya benki hiyo.

Dk. Mpango alipokea hundi hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB, Dk. Ally Laay.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mpango aliipongeza benki hiyo kwa kutoa gawio kwa serikali pamoja na kupata matokeo mazuri ya fedha kwa mwaka 2019 ambayo yamewezesha kuongezeka kwa gawio kwa wanahisa, ikiwamo serikali.

“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa serikali kuwa CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii,” alisema.

Dk. Mpango alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitasaidia utekelezaji wa miradi ambayo serikali imeiainisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2020/2021.

“Kipekee kabisa niipongeze bodi, menejimenti na wafanyakazi wote wa CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” aliongezea Dk. Mpango.

Pia aliipongeza CRDB kwa matokeo mazuri ya fedha iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu kutokana na ongezeko la faida kwa asilimia 15 kufikia Sh. bilioni 70.4 kutoka TZS bilioni 61.1 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa taasisi za fedha katika maendeleo ya taifa, Dk. Mpango aliipongeza CRDB kwa kupunguza riba katika mikopo ili kuchochea shughulia za maendeleo nchini.

“Niwapongeze kwa kupunguza riba katika mikopo, hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu cha serikali kwa mabenki (benki) nchini. Niyasihi (nizisihi) mabenki (benki) mengine (nyingine) kufuata nyayo hizi za benki ya CRDB,” alisema Dk. Mpango.

Dk. Laay alisema gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh. bilioni 120.1 baada ya kodi ambayo CRDB na kampuni zake tanzu imeipata katika mwaka wa fedha 2019. Pia alisema kuwa benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.

“Katika mkutano wa wanahisa uliofanyika kidijitali Juni, mwaka huu, wanahisa wa benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la Sh. 17 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 112.5, hivyo kufanya gawio la mwaka huu kufikia Sh. bilioni 44.4,” alisema Dk. Laay.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, alimhakikishia Dk. Mpango kuwa CRDB kupitia kauli mbiu yake ya “Tupo Tayari” itaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha.

Alisema benki hiyo imejikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ya kutolea huduma kama CRDB Wakala, SimBanking, SimAccount na Internet banking ambayo humsaidia mteja kupata huduma kwa urahisi, unafuu na haraka.

Akipokea gawio kutokana na uwekezaji wa halmashauri za Mbinga, Lindi, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, alizihimiza halmashauri zingine nchini kuweka katika hisa ili kupanua wigo wa mapato.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Vijana, Jenista Mhagama, alipongeza mifuko ya jamii ya PSSSF, NSSF na ZSSF kwa uwekezaji ndani ya CRDB huku akiwataka viongozi wa mifuko hiyo kutumia gawio walilopata kuboresha utendaji kazi ili kunufaisha wanufaika wa mifuko hiyo.

Habari Kubwa