Serikali yaridhishwa uandikishaji wanaoanza kidato cha kwanza

18Jan 2022
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Serikali yaridhishwa uandikishaji wanaoanza kidato cha kwanza

WAKATI jana shule za msingi na sekondari zikifunguliwa, serikali imeeleza kuridhishwa na uandikishaji na kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza katika mwaka huu wa masomo.

Vile vile, imesisitiza kuanza mchakato wa kuajiri walimu na kuongeza matundu ya vyoo katika shule za umma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, aliyasema hayo jana jijini hapo wakati wa ziara ya kutembelea shule wilayani Chamwino kwa lengo la kujionea wanafunzi walioripoti.

Alisema baada ya serikali kukamilisha madarasa kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeanza mazungumzo na Wizara ya Utumishi kwa ajili ya kuajiri walimu na ujenzi wa matundu ya vyoo.

Aliwaagiza wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na maofisa elimu wa ngazi zote, kusimamia kazi iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanafunzi waliofaulu wanaripoti na wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kusimamia miundombinu hiyo.

"Rais Samia amehakikisha kunakuwa na mahali pazuri pa kusomea kama hapa Shule ya Sekondari Chamwino, nielekeze wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi, maofisa elimu ngazi zote wahakikishe wanafunzi waliofaulu wanaripoti shuleni na wale wenye umri wa kuanza shule waandikishwe," alisema.

Bashungwa aliziagiza halmashauri kutumia sehemu ya mapato ya ndani kujenga nyumba za walimu na kupunguza sehemu ya fedha kutoka Serikali Kuu kuelekeza katika ujenzi wa nyumba hizo lengo likiwa ni kuweka mazingira mazuri.

"Si hivyo tu, pia Rais Samia anawajali walimu wake, hivyo tumejipanga kuhakikisha tunalinda na kutetea maslahi ya walimu ikiwamo kupandishwa madaraja," alisema.

Pia Bashungwa alimwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, shule zote zisizo na hati na mpya maeneo yake yanapimwa na kuwa nazo.

Naye Katibu Tawala Wilaya ya Chamwino, Neema Nyerege, alisema Wilaya ya Chamwino ilipokea Sh. bilioni 2.9 kwa ajili ya kujenga madarasa 146 ya sekondari na vituo shikizi.

Habari Kubwa