Serikali yaridhishwa utafiti wa mbegu

12Aug 2020
Welingtone Masele
Tabora
Nipashe
Serikali yaridhishwa utafiti wa mbegu

SERIKALI imesema imeridhishwa na utafiti wa mbegu za mazao unaofanywa na taasisi za kilimo mikoa ya Tabora na Kigoma.

Akizungumza katika kilele cha maonyesho ya wakulima Nanenane, Kanda ya Magharibi, katika uwanja wa Fatma Mwassa, eneo la Ipuli mjini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi, Thobias Andengenye, alisema utafiti na elimu iliyotolewa na taasisi hizo vimeleta tija kubwa kwa wakulima.

Alisema kuanzishwa kwa vituo vya utafiti wa mazao kumekuwa msaada mkubwa kwa wakulima kutokana na ushauri mzuri wa kitaalamu, ubunifu na dhamira njema ya kuwainua wakulima.

Alitaja taasisi zilizoleta mageuzi sekta ya kilimo na kuanza kunufaisha wakulima kuwa ni pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa (TACRI) na kampuni ya Felisa.

Alitoa wito kwa wadau na taasisi mbalimbali nchini kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika kanda hiyo ikiwamo kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima.

Alisisitiza kuendelea kuimarishwa kwa bodi za mazao na kuboreshwa kwa miradi ya ufugaji samaki katika halmashauri zote za mikoa hiyo huku akiwataka wananchi kutumia ipasavyo ujuzi na elimu waliyopata katika maonyesho hayo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Philemon Sengati, alisema ndoto yake ni kuona maonyesho ya wakulima katika kanda hiyo yanakuwa ya mfano wa kuigwa na kanda zingine na ikiwezekana mwakani kitaifa yafanyikie hapo.

Pia, dhamira yake ni kuona maonyesho ya ukanda huo yanakuwa mashamba darasa na bidhaa zote zinazoletwa ziwe na tija kubwa kwa wakulima, jamii, nchi na mataifa mengine kwa ujumla.

Habari Kubwa