Serikali yashauriwa kuinua elimu Zanzibar

09Aug 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Serikali yashauriwa kuinua elimu Zanzibar

WADAU wa Elimu wameitaka Serikali kuajiri walimu wenye sifa na uwezo ili kuinua ubora wa uelewa kwa wanafunzi pamoja na kuweka mazingira bora ya shule.

waziri wa elimu na mafunzo ya amali zanzibar, riziki juma pembe.

Wakizungumza katika majadiliano ya mbinu za kukuza kiwango cha elimu Zanzibar jana, wadau hao walisema jitahada zinahitajika pia katika kukuza uwelewa haswa kwa wazazi, juu ya umuhimu wa watoto kupata elimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mshauri Khamis alisema uandikishaji wa wanafunzi wapya shuleni na wale ambao wanaendelea kupata elimu uendane sambamba na uwepo wa mazingira bora ya kupata elimu hiyo ndipo watoto wataweza kufanya vizuri kimasomo.

Aidha, Khamis aliitaka serikali kuhakikisha inaboresha maslahi ya walimu ili wawe na ari ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

"Walimu watakapotimiziwa mahitaji yao yote, ikiwamo posho na vitendea kazi, kutajenga ari ya ufundishaji kwa walimu hao,” alisema Khamis.

Aidha, Khamis aliitaka Serikali ihakikishe inajenga uwelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa watoto wenye ulemavu kupata elimu.

Alisema uandikishwaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ni mdogo ambapo mwaka 2006 ilikuwa asilimia 1.2 na mwaka 2014 ni asilimia 1.4, kiwango ambacho bado hakiridhishi.

“Inaonesha kuwa watoto wengi wenye ulemavu wanafichwa majumbani bila ya kupatiwa elimu wakati ni haki yao ya msingi.”Khamis alisema.

Habari Kubwa