Serikali yashtuka

24Nov 2016
Daniel Mkate
Dodoma
Nipashe
Serikali yashtuka
  • Ni kuhusu utumbuaji majipu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewaonya na kuwaagiza viongozi katika wizara, mikoa, wilaya, idara za serikali, halmashauri na taasisi zote za serikali kuacha tabia ya kuwanyanyasa, kuwashusha vyeo ama kusimamishwa wafanyakazi bila kufuata sheria na kanuni za kazi.

Aidha, Majaliwa pia ameonya dhidi ya tabia ya kuwaweka ndani kiholela watumishi wa umma kunakofanywa na viongozi hao.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) mjini Dodoma jana, Majaliwa alisema wakuu hao wanatakiwa kuzingatia utawala wa sheria katika kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi.

“Hata hivyo, rai yangu kwa wafanyakazi kupitia vyama vyao, kutakiwa kutekeleza majukumu yao kwa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu wa hali ya juu kwenye maeneo yao ya kazi,” alisema Majaliwa.

Alisema nidhamu ya kazi katika maeneo mengi imeporomoka kutokana na wafanyakazi kutotimiza wajibu wao ipasavyo huku wengi wao wakiwa wabadhirifu wa mali na fedha za umma hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

“Napenda kusisitiza, serikali ya awamu ya tano haiweza kufumbia macho watumishi wanaojishughulisha na ubadhirifu, ufisadi wa fedha za umma… hawa lazima tutakomaa nao,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evelisit Ndikilo, Oktoba 29 alimtumbua katikati ya sherehe, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nasibugani iliyopo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Hilali Bwagidu.

Kiongozi huyo wa serikali alichukua uamuzi huo wakati wa sherehe ya kuwatunuku vyeti vijana wazalendo waliofyatua matofali ya shule hiyo, sherehe iliyohudhuriwa na Waziri wa Elimu Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.

Kabla ya kumkaribisha Prof. Ndalichako aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa alitangaza kumtumbua jipu mwalimu huyo kutokana na kile alichodai kupata taarifa kuwa toka vijana hao wazalendo wafike katika shule hiyo, hawakuwa na ushirikiano wowote kutoka kwa mkuu huyo wa shule.

Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na shule hiyo, walidai kwa nyakati tofauti kuwa mwalimu huyo hakuonekana kwa kipindi kirefu shuleni kutokana na kuuguza mmoja wa wanafamilia yake jijini Dar es Salaam.

Mamlaka ya uwajibishaji ya Mkuu wa Shule ni Mkurugenzi wa Wilaya (DED), hata hivyo.

Katika tukio jingine, kwa mfano, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alimwagiza Mkuu wa Polisi kumkamata na kumfungulia mashtaka Mhasibu Mkuu wa Halmashauri ya wilaya hiyo mkoani Arusha, Issa Mbilu, kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa Sh. milioni 84.

Akizungumza juu ya agizo hilo la kukamatwa Mhasibu huyo, Chongolo alisema uamuzi huo unatokana na upotevu wa fedha hizo zilizorudishwa na benki zilizokuwa zilipwe kwa watumishi hewa na wale waliokuwa na matatizo kazini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa alitangaza kumsimamisha kazi muuguzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Patricia Chisoti Oktoba 21 kwa madai ya uzembe uliosababisha kifo cha mtoto mchanga.

Oktoba 8, Meneja wa Mamlaka ya Maji katika mji wa Kongwa mkoani Dodoma, Tshabonga Leo alisimamishwa kazi na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi kwa madai ya kushindwa kusimamia upatikanaji wa maji.

Aidha, Mwezi uliopita pia, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata Diwani wa Kata ya Lumanyata pamoja na wenyeviti na watendaji wa vijiji kwa madai ya kushindwa kubaini shamba la bangi katika kata hiyo.

ASILIMIA 100
Makamu wa Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Flaviana Charles alisema anaunga mkono marufuku ya Majaliwa kwa asilimia 100 na kwamba Watanzania wamuunge mkono Waziri Mkuu.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004, kila muajiriwa, mtumishi amepewa nafasi ya kujieleza na ndio maana hata watuhumiwa wa ujambazi wanapokamatwa hutuhumiwa hadi sheria itakapo watia hatiani.

“Utaribu uliokuwa unafanyika haukutumia sheria na haki, naamini nchi haiwezi kuendeshwa bila kuzingatia utawala wa kisheria, kila muhimili unapaswa kujiendesha kwa kufuata taratibu hizo na ndio utawala bora,” alisema Charles.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema ameunga mkono tamko la Waziri Mkuu, akisema hatua hiyo itaondoa uonevu.

Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa serikali, wanasiasa na wafanyakazi wote, kuwajibika na kuheshimu sheria za nchi zikiwamo zinazotawala mahusiano ya waajiri na waajiriwa sehemu zao za kazi.

Alisema huu ni wakati wa kubadilika kifikra na kiutendaji, kwani kila mwajiriwa anatakiwa kutimiza wajibu wake wa kufanya kazi ili kuepukana na migogoro isiyokuwa na ulazima.

Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, alisema lipo tatizo la ajira sehemu nyingi ambazo wafanyakazi wanafanya kutokana na waajiri kutowapa mikataba ya kazi.

Mhagama alisema maagizo yatakayotolewa na Waziri Mkuu ni lazima waajiri wayafanyie kazi na watumishi waweze kunufaika na kile wanachokifanya.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki, alisema serikali ya awamu ya tano inathamini sana vyama vya wafanyakazi.

Alisema uthamini huo unatokana na kufanikiwa kuwapandisha vyeo wafanyakazi 343,689 katika kipindi cha 2011 hadi 2016.

“Changamoto iliyopo ni watumishi wengi kutokidhi vigezo vya kuwawezesha kupanda vyeo," alisema Kairuki.

"Wito ni wafanyakazi ambao hawajapanda vyeo kwa muda mrefu kuhakikisha wanapewa kipaumbele cha kushiriki mafunzo mbalimbali yanapotolewa.”

KATIBU MKUU
Nicholaus Mgaya, katibu mkuu wa TUCTA, alisema katika kuelekea Tanzania kuwa nchi ya viwanda, serikali inatakiwa kuangalia haki ya mfanyakazi.

Mgaya alisema mambo mengi ambayo walikuwa wakiyapigia kelele miaka mingi, wanashukuru serikali ya awamu ya tano imeweza kuyatatua baadhi ya mambo yanayowakabili wafanyakazi.

Alitaja baadhi ya mambo yaliyoweza kutatuliwa ni kupunguza kodi ya mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na vita vya ufisadi na ujangili.

Habari Kubwa