Serikali yashtukia hatari wanyama kutoweka

25Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe Jumapili
Serikali yashtukia hatari wanyama kutoweka

SERIKALI imeitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) kusimamia kisayansi sekta ya wanyamapori ikiwamo ya kuhakikisha wanyama walio hatarini kutoweka, wakiwamo mbwa mwitu, faru weusi na duma, wanaendelea kudumu.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu picha na mtandao

Mkakati huo wa serikali umebainishwa kwa nyakati tofauti na viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii waliofanya ziara maalumu kwa nyakati tofauti wiki hii katika taasisi hiyo yenye makao makuu yake jijini hapa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, katika ziara yake, aliitaka taasisi hiyo kufanya utafiti juu ya tishio la kutoweka kwa faru weusi ambalo kwa sasa limeongezeka kutokana na watoto wao kuliwa na fisi madoa katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Kanyasu alisema fisi hao wamekuwa tishio hata kwa binadamu ambapo tayari wananchi watatu wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na bonde la Ngorongoro, wameuawa kwa kuliwa na fisi.

"Kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kufanya utafiti kwani hii si hali ya kawaida. Nimeelezwa hao fisi pia ni hatari hata kwa duma kwani wanaua na kuwala watoto wa wanyama hao," alisisitiza.

Kanyasu aliihakikishia taasisi hiyo kupata bajeti ya utafiti kutoka kwa wadau, wakiwamo Shirika la Hiafadhi za Taifa (Tanapa) na NCAA ambao sheria inawataka kutoa asilimia tatu ya mapato yao kwa kila mwaka wa fedha.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda, alisema katika serikali ya awamu ya tano, suala la utafiti litapewa kipaumbele na kuitaka Tawiri kuhakikisha inaongeza nguvu na kujipanga zaidi ili iwe bora kama ilivyo kwa taasisi kama hizo zilizoko katika nchi zilizoendelea.

"Bahati mbaya utafiti katika nchi yetu haupewi kipaumbele, unaonekana kama vile ni anasa. Serikali kwa sasa haitakubali hali hiyo iendelee na uzuri ni kwamba kiongozi wetu mkuu, Rais John Magufuli ni mwanasayansi,"alisema.

Miongoni mwa dosari katika utafiti nchini ambazo Prof. Mkenda alizianisha ni pamoja na ugumu katika kupata kwa usahihi idadi kamili ya wanyamapori.

"Utafiti na ugunduzi sasa ni lazima ufanywe na watafiti wa Kitanzania badala la kila tatizo linapotokea tusubiri watafiti kutoka nje ya nchi. Kwa sasa hilo halitakubalika na Tawiri lazima mchukue jukumu lenu," alisisitiza Prof. Mkenda.

Hata hiyo, Prof. Mkenda aliipongeza taasisi hiyo kwa kutoka machapisho 57 kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Novemba, mwaka huu, yakiwemo 28 kwenye makongamano ya kisayansi, taarifa maalumu za kisayansi 16 na kitabu kimoja cha ikolojia ya barabara ya Serengeti kaskazini.

Alimpongeza mtafiti wa taasisi hiyo, Dk. Develent Mtui, kwa kugundua aina mpya ya vipepeo katika bonde la Kihansi ambao wamepewa jina la Charaxes Mtuiae.

Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Dk. Simon Mduma, alisema tayari wameanza utafiti wa marejeo ya tathimini ya athari kuu za kiikolojia kwenye mradi wa umeme wa bonde la Mto Rufiji wa Stieglers Gorge, ndani ya pori la akiba la Selous.

Alisema matokeo ya awali yanaonyesha kuwa kuna jamii 45 katika familia 21 za wanyama wakubwa katika eneo hilo, zikiwamo saba zilizoko katika uangalizi maalumu kutokana na kuwa katika hatari ya kutoweka. Alizitaja jamii hizo kuwa ni mbwa mwitu, pundamilia, tembo, simba, chui, kiboko na twiga.

Aidha, Dk. Mduma alisema pia wamebaini jamii za wanyama wadogo 13, ndege 190, wanyama wanaoishi nchi kavu na majini, wanyama watambaao tano na jamii ya athropoda saba 7 pamoja na jamii nne za ndege walioko kwenye hatari ya kutoweka endapo hawatahifadhiwa.

Dk. Mduma alisema wanaendesha utafiti wa tatizo la kuliwa kwa watoto wa faru kunakofanywa na fisi katika mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na tayari wamefunga kamera-mitego za kidigitali zipatazo 100.

Alisema kuwa utafiti wa awali unaonyesha kwamba idadi ya fisi imeongezeka kutoka 300 kwa mwaka 2002 hadi takribani fisi 600 kwa mwaka 2017

Kwa mujibu wa Dk. Mduma, mbwa mwitu waliopotea katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wameanza kurejea na sasa kuna makundi manane yenye mbwa hao zaidi ya 500.

Tawiri ilianzishwa mwaka 1980 wakati huo ikijulikana kama Taasisi ya Utafiti Wanyamapori ya Serengeti (SWRI) kabla ya mwaka 1999 kubadilishwa jina na kuitwa jina la sasa ili kukidhi sura ya kitaifa.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa Tawiri ni kuendesha na kusimamia utafiti wa wanyamapori nchini, kutoa takwimu na ushauri wa kitaalamu ili kuiwezesha serikali na wadau wa wanyamapori kusimamia uhifadhi endelevu wa sekta hiyo.

Habari Kubwa