Serikali yasikia kilio cha wafanyakazi

11Jun 2021
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali yasikia kilio cha wafanyakazi

SERIKALI imesikia kilio cha wafanyakazi, baada ya jana Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, kutangaza punguzo la kodi ya mishahara (PAYE) kutoka asilimia tisa hadi nane.

Akiwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22, Waziri Nchemba, alisema serikali inatarajia kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kwa kiasi hicho.

“Hatua hii ni mwendelezo wa juhudi za serikali za kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi. Kiwango hicho kimepunguzwa kutoka asilimia 11 mwaka 2015/16 hadi asilimia nane itakayoanza kutekelezwa mwaka 2021/22,” alisema.
Waziri Nchemba pia alitangaza kufuta tozo ya asilimia sita iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya mkopo wa elimu ya juu kwa wanufaika.

Pia alitangaza serikali kutenga Sh. bilioni 449 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 92,619.

MADIWANI

Waziri Nchemba alisema kuanzia mwaka 2021/22 serikali kuu itaanza kulipa posho za madiwani za kila mwezi moja kwa moja kwenye akaunti zao kwa halmashauri zenye uwezo mdogo kimapato.

Hata hivyo, alisema kwa halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa  wa kimapato zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za madiwani kupitia kwenye akaunti zao.

MAOFISA TARAFA

Kuhusu maofisa tarafa, Waziri Nchemba alisema kuanzia mwaka 2021/22, serikali kuu itaanza kulipa posho ya Sh.100,000 kwa mwezi kwa kila ofisa tarafa ili kumudu gharama za mafuta na matengenezo ya pikipiki.

WATENDAJI KATA

Kuhusu maofisa kata, Waziri Nchemba alisema serikali itaanza kulipa posho ya Sh.100,000 kwa mwezi kwa kila mtendaji kata kupitia mapato ya ndani ya halmashauri yaliyokuwa yakitumika kulipa madiwani.

MIFUKO HIFADHI YA JAMII

Waziri Nchemba alisema kumekuwapo na changamoto za muda mrefu za ulipaji wa mafao ya wazee kunakosababishwa na ufanisi mdogo wa mifuko ya hifadhi ya jamii katika kuhudumia wastaafu.

“Hali hiyo kwenye mifuko yetu 23 imechangiwa, pamoja na mambo mengine, na uwepo wa madeni ambayo mifuko inaidai serikali na hivyo kusababisha wastaafu wetu kukosa au kusubiri kwa muda mrefu ili kulipwa mafao yao,” alisema.

Alisema Wizara ya Fedha na Mipango kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kukamilisha zoezi la kitaalamu ili kujua hali halisi ya madeni na namna bora ya kulipa madeni hayo.

“Napendekeza kulipa madeni yanayodaiwa na mifuko kwa kutenga fedha kwenye bajeti na kutumia utaratibu wa kutoa hatifungani maalum isiyo taslimu zitakazoiva kwa nyakati tofauti kuanzia miaka miwili hadi 25,” alisema.

Alisema utaratibu wa hatifungani una faida mbalimbali zikiwamo kuipa serikali nafasi ya kibajeti ya kuendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo, kuiwezesha Serikali kuyatambua madeni hayo kwenye kanzidata ya madeni na kuzuia madeni hayo kuendelea kuongezeka kulingana na tathmini ya thamani ya madai.

Alisema utaratibu huo pia utaboresha mizania ya hesabu na mtiririko wa mapato yanayotokana na riba ya hatifungani hizo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Waziri Nchemba alisema hatua hiyo itakwenda kumaliza tatizo la wazee kudai haki yao kwa damu na machozi yaliyodumu kwa muda mrefu.

Alisema serikali imepokea malalamiko kuhusu kucheleweshwa kwa michango ya watumishi kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na baadhi ya ofisi za Serikali kutopeleka kabisa michango hiyo.

Habari Kubwa