Serikali yataifisha pamba tani 26 iliyokamatwa ikitoroshwa 

14Aug 2019
Happy Severine
BARIADI
Nipashe
Serikali yataifisha pamba tani 26 iliyokamatwa ikitoroshwa 

Baada ya kukamatwa kwa lori aina ya skania yenye namba za usajili T-917 BCN likiwa limebeba tani zaidi ya 20 za pamba inayodaiwa kuwa ni ya magendo,hatimaye  Serikali ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu imeamua kuitaifisha pamba hiyo.

mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga (katikati) akitoa maamuzi ya kuitaifisha pamba tani 26 zilizonunuliwa kimagendo.

Lori hilo ambalo lilikamatwa jana Agosti 13, mwaka huu katika  kijiji cha Dutwa Wilayani Bariadi Mkoani hapa, lilikutwa majira ya saa tano usiku likisafirisha pamba hiyo bila kibali maalumu huku ikiwa haijulikani wapi inapelekwa na wapi imenunuliwa.  

Akitoa maamuzi ya kuitafisha pamba hiyo leo Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga amesema kuwa uchunguzi umeonyesha kuwa pamba hiyo ilinunuliwa kwa njia ambayo si ya halali kwa bei ya sh.700 hadi 900 kwa kilo kutoka moja kwa moja kwa wakulima.

Kiswaga amesema kuwa wakati serikali ikipambana na watu wanaonunua pamba kwa njia za kimachinga, bado wapo wafanyabishara wa zao hilo wanaendelea kupiga vita juhudi hizo kwa kuendeleza biashara hiyo na kuwanyonya wakulima.

"Baada ya wahusika kushindwa kujitokeza, sasa kama Mkuu wa Wilaya hii ya Bariadi nachukua uamuzi wa kuitaifisha pamba hii na tunaenda kuiuza kwenye viwanda vya kuchambua pamba Leo hii na pesa zote zitapelekwa kununua vifaa vya kukamilisha ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Simiyu," amesema Kiswaga.

Amesema kuwa Ofisi yake haitalala ili kuhakikisha inapambana na biashara hiyo lengo likiwa ni kuwasaidia na kuwanufaisha  wakulima wa zao hilo.

Ameongeza kuwa pamba hiyo ina thamani ya zaidi ya sh.Milioni 10, na  baada ya kuuzwa uchunguzi utaendelea kujua nani mhusika mkuu huku gari akieleza kuwa itaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi mpaka muhusika atakapojitokeza.

Habari Kubwa