Serikali yatakiwa kuboresha mazingira ya walimu vijijini

28Nov 2016
Rose Jacob
MWANZA
Nipashe
Serikali yatakiwa kuboresha mazingira ya walimu vijijini

SERIKALI imeombwa kuwaboreshea mazingira ya kufanyia kazi walimu wa vijijini, ikiwamo maji, umeme na nyumba.
Hayo yalisemwa jana na Mwalimu wa Shule ya Msingi Kabusungu,

Penina Mollel, wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utafiti wa kiwango cha elimu, uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Twaweza, iliyoonyesha katika wilaya ya Ilemela, kukabiliwa na changamoto ya watoto kutokufika shuleni kutokana na wazazi kuwafanyisha kazi za nyumbani.

Alisema walimu wa vijijini wanapata wakati mgumu kutokana na mwalimu mmoja kufundisha masomo matano kwenye darasa lenye wanafunzi 80 hadi 100, wakati mjini somo moja linafundishwa na walimu watatu.

“Upungufu wa walimu pamoja na uhaba wa mahitaji muhimu ni kikwazo kwa elimu nchini hususani vijijini, unakuta mwalimu mmoja anafundisha masomo zaidi ya matatu kwenye darasa lenye watoto 80 hadi 100,” alisema Molell.

Mwalimu Mary Mkakaro, alisema sababu za kushuka kwa elimu ni kuajiri walimu wenye umri mdogo ambao wanalenga masilahi yao badala ya watoto.

Meneja utetezi Twaweza, Annastazia Rugaba, aliwataka walimu kuacha tabia ya kuona serikali imewatenga na kuamua kufanya biashara zao, huku kiwango cha elimu kikishuka kila mwaka.

“Hatukatai upungufu wa walimu upo, lakini ni kwa baadhi ya shule na sio zote, katika utafiti tulioufanya Wilaya ya Ilemela walimu 72 ndio walioudhuria darasani ni sawa na asilimia 2.2 tu, ukiwauliza ni kwa nini mahudhurio hafifu, utasikia visingizio ni vingi vya ugonjwa, kufiwa hali hii inaturidisha nyuma,” alisema.

Hata hivyo, Mkurungenzi wa Education Developing and Facilitating Organization (EDFO), Noel Kihoza alisema, wanataka kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati, lakini kwa takwimu ambazo zinafanywa na wadau mbalimbali wa elimu, haziridhishi na kuwataka kuongeza juhudi za ufundishaji.

Habari Kubwa