Serikali yatangaza kampeni kurudisha fuvu la shujaa

19Apr 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Serikali yatangaza kampeni kurudisha fuvu la shujaa

SERIKALI imetangaza kampeni ya kurudisha fuvu la shujaa mwanamke, Leti Hema, kutoka Kabila la Wanyaturu ambaye kichwa chake kilikatwa na Wajerumani kisha kupelekwa Ujerumani wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Kampeni hiyo ilitangazwa bungeni jijini Dodoma jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alipowasilisha hotuba kuhusu makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

"Alipouawa shujaa huyo, wakoloni hawakuridhika waliamua kukata kichwa chake na kukipeleka Ujerumani kwa uchunguzi wa kina kubaini kama alikuwa na uwezo maalum wa kibaiolojia wa kufundisha wadudu wadogo wenye ubongo mdogo kama nyuki," Dk. Mwakyembe alisema.

Waziri huyo aliendelea kueleza kuwa shujaa huyo alisimama kidete kuzuia utawala wa Kijerumani kwa zaidi ya miaka mitatu akitumia makundi ya nyuki waliowang'ata wazungu pekee.

Alisema nyuki hao waliwazuia Wajerumani kufika kwenye Kilima cha Ng'ongo Ipembe na maeneo yanayozunguka eneo la sasa la Singida Mjini.

"Mbali na hayo, shujaa huyo alionyesha miujiza alipokutana na Wajerumani kwa mazungumzo yaliyovunjika kwa kukaa juu ya ncha kali ya mkuki badala ya kigoda cha kawaida," Dk. Mwakyembe alisema.

Waziri huyo alisema shujaa huyo na wengine walioshiriki harakati za ukombozi wakiwamo Mtemi Isike wa Tabora aliyepigana na Wajerumani kwa zaidi ya miaka minne na Nduna Mkomanile wa Wangoni, hawajaandikwa wala mchango wao kuthaminiwa katika historia.

Alibainisha kuwa mbali na kufufua kampeni ya kurejesha nchini fuvu hilo, wizara yake itasimamia kampeni ya kuhimiza watafiti kuandika upya historia ya ukombozi wa taifa.

Dk. Mwakyembe alisema serikali inaendelea kuandaa sheria itakayosimamia uhifadhi na uendelezaji wa maeneo yenye historia ya ukombozi wa nchi na Afrika.

"Vilevile, uliandaliwa mpango wa kikanda wa miaka mitano wa utekelezaji wa programu ya pamoja na mpango wa kitaifa wa miaka mitano ambao umewasilishwa kwa wadau wa ndani na nje ya nchi kwa utekelezaji wa vipaumbele na malengo ya mipango hiyo," alisema.

Dk. Mwakyembe aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/20, Baraza la Kiswahili (Bakita) litaandaa vipindi 600 vya redio na televisheni vya kuelimisha umma kuhusu matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili.

Pia kutakuwa na usanifishaji istilahi 300 za nyanja mbalimbali, kutambua na kusajili taasisi na vituo 20 vinavyofundisha Kiswahili kwa wageni na kuongeza matini za maneno 500,000 ya kongoo la Kiswahili.

Alitaja majukumu mengine ni kuendelea kusajili wataalamu wa Kiswahili katika kanzidata iliyoanzishwa, kuendesha semina 10 kwa waandishi na watangazaji wa redio na televisheni.

Ili kutekeleza majukumu ya wizara katika mwaka ujao wa fedha, Dk. Mwakyembe aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh. bilioni 30.879. Kati yake, Sh. bilioni 15.483 ni mishahara, Sh. bilioni 9.396 ni matumizi mengineyo na Sh. bilioni sita za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Habari Kubwa