Serikali yatenga bilioni 45 uwekaji anuani za makazi

17Oct 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe Jumapili
Serikali yatenga bilioni 45 uwekaji anuani za makazi

SERIKALI imetenga bilioni 45 kwa ajili ya kukamilisha uwekaji wa anuani ya makazi na posti kodi (post code) kwenye nyumba zilizoko kwenye halmashauri zote 194 nchini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Ashatu Kijaji,wakati wa ziara ya kuona utekelezaji wa zoezi zima la anuani za makazi na post code jijini  Mwanza ambalo lilikuwa ni sehemu ya kujifunzia kabla ya kuanza kwa zoezi hilo nchi nzima.

Anasema mpango huo umeanza kwa kufanyiwa majaribio katika Halmashauri ya jiji la Mwanza ambapo utekelezaji wake umefanikiwa kwa kiwango kikubwa hivyo zoezi hilo litaendelea katika Halmashauri 184 za Tanzania Bara na Halmashauri 10 za Tanzania visiwani.

Anasema lengo kuu ni kuhakikisha kila mtaa unakuwa na jina lake huku kila nyumba ikiwa na namba yake hiyo itasaidia kurahisisha ufanisi na utendaji kazi wa serikali ndani ya jamii sanjari  na kusaidia  kufikia uchumi wa kidigitali.

Anaeleza kuwa serikali ina malengo makubwa na wananchi wake huku dhamira yake ukiwa ni kurahishisha huduma na ziweze kufikia kirahisi zaidi pindi wanapozihitaji .

Aidha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula ameeleza kuwa kazi hii ya utekelezaji wa anwani za makazi nchini nzima utatekelezwa na wananchi wenyewe waliopo kwenye maeneo hayo na itatoa ajira kwa wananchi hao na ametoa rai kwa wananchi kuwa tayari kujitokeza kutekeleza mpango huu wa anwani za makazi na postikodi

Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu wa Anuani za Makazi na Posti KodiHalmashauri ya Jiji la Mwanza,Mosse Seleki amesema katika utekelezaji wa mradi huo wamefanya vitu vitatu ambapo jumla ya nyumba 108000,zimefungwa namba za nyumba ,nguzo 5800 zenye vibao vya majina ya mtaa vimemekea huku  nyumba 98,000 zimeingizwa kwenye mfumo wa anwani za makazi wa simu ya mkononi mradi huo umefanyika kwenye mitaa yote 175 ya jiji la Mwanza.

Naye Mkuu wa Mkoa Mhandisi Robert Gabriel anaeleza kuwa  wananchi wana kiu ya kujulikana kwa kuwa sasa mitaa yao ina majina na nyumba zao zina namba ambapo mwananchi analetewa mzigo wake pale alipo kwa kuwa sasa anatambulika mahali anapoishi na kufikiwa kirahisi.

Anaeleza kuwa kuna changamoto mbalimbali zinazojitokeza mkoani humo ikiwemo nyumba kuungua hivyo mkazi wa eneo hilo akiomba msaada kwa kutaja mtaa na namba ya nyumba watapata huduma Moja kwa Moja na uharaka zaidi .

Ameongeza kuwa hiyo ni fursa kwao Mkoa huo hivyo vijana, vikundi vyenye uzoefu wakutengeneza vibao hivyo ambavyo kwa sasa vinatokea Dar es Salam wajitokeze kwa sababu mradi huo utafika kwenye Wilaya zote.

" Vijana msilalamike hakuna ajira tunawaomba mje mtuambie vibao kama hivi mtatengeneza kwa gharama zipi zikiwa zipo chini mtapatiwa tenda hiyo vijana wote mnaohitaji fursa mje kwenye ofisi yangu Ili tujadiliane" alieleza Gabriel

Diwani wa kata ya Nyamagana, Biko Kotecha akizungumza kwa niaba ya wananchi wake ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi kwa kuwa mradi huu una tija kwao.

Habari Kubwa